DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania waendelee kujiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi kwani ndiyo njia sahihi ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.
Amesema kuwa,takwimu za Wizara ya Afya nchini zinaonesha hospitali zina idadi kubwa ya wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza hivyo hamasa na msisitizo uliotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kufanya mazoezi haina budi kupewa kipaumbele na wananchi wote.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito huo leo Jumamosi, Mei 18, 2024 katika Mbio za Pugu (Pugu Marathon) zilizolenga Kuendeleza kituo cha Hija cha Pugu kilichoanzishwa na Wamisionari wa Shirika la Wabenediktini kutoka Ujerumani waliofika Dar es Salaam mwaka 1888 kuwa kituo cha kimataifa.
“Pamoja na kusisitiza mazoezi kama moja ya njia ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukizwa, tuendelee kuelimishana pia kuhusu ulaji sahihi wa vyakula (healthy eating) na kubadili mitindo ya maisha ambayo ina athari katika afya zetu.”
Waziri Mkuu amezielekeza taasisi za Serikali, dini na binafsi kuweka utaratibu wa kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kushiriki katika mazoezi ambayo yanatumika kujiimarisha wenyewe kiafya na kusaidia wahitaji mbalimbali.


