KATAVI-Mei 9, 2024 katika Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika mbele ya Mheshimiwa Sydney Nindi, Hakimu Mfawidhi imefunguliwa kesi ya Jinai namba CC. 12307/2024 ya Jamhuri.
Ni dhidi ya Bw. Pius Emmanuel Lyambise na Nestori Fransisko Gabulieli ambao ni mgambo wa Kijiji cha Majalila, Kata ya Majalila, Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.
Watuhumiwa hao wawili wanashtakiwa kwa kuomba hongo ya shilingi 200,000 kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya Mwaka 2022.
Akisoma hati ya Mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Amos Mwalwanda amesema, washtakiwa hao mnamo tarehe 25 Aprili, 2024 waliomba hongo hiyo kutoka kwa
Devidi Elias Shem na Alphans Japhet Bwangaro wa Kijiji cha Kazima, Kata ya Kazima, Wilaya ya Mpanda ili wawaachie.
Ni baada ya kuwakamata wakisafirisha mbao kutoka Tanganyika kwenda Mpanda bila kibali kinyume na utaratibu.
Washtakiwa wamekana kosa na wamepelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutekeleza masharti ya dhamana.
Tags
Habari
Mahakamani
Mgambo wa Kijiji
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania