Mgogoro wa mipaka Pori la Akiba Liparamba watatuliwa, wananchi washukuru

NA BEATUS MAGANJA

JITIHADA za Serikali za kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya Hifadhi na wananchi zinaendelea kuzaa matunda baada ya kutatua mgogoro uliodumu zaidi ya miaka 20 baina ya Pori la Akiba Liparamba lililopo mkoani Ruvuma na vijiji vitano vinavyozunguka hifadhi hiyo.
Hayo yamebainika Mei 28, 2024 katika ziara ya kuelezea namna TAWA ilivyotekeleza kikamilifu maagizo ya Serikali na mapendekezo ya Baraza La Mawaziri la Kisekta (BLM) kuhusiana na utatuzi wa mgogoro huo.Akizungumzia mgogoro huo, Kamanda wa Hifadhi hiyo, Annzikar Joseph Lyimo amesema Pori la Akiba Liparamba lilikuwa na mgogoro wa mipaka kati yake na vijiji vinavyolizunguka ambavyo ni Ndondo, Mseto, Mipotopoto, Liparamba na Mitomoni.

Mgogoro unaotajwa kudumu zaidi ya miaka 20 lakini ulitatuliwa Mwaka 2023 ikiwa ni matokeo ya ziara ya Mawaziri wa Wizara nane wa kisekta ya kutembelea maeneo yenye migogoro ya matumizi ya Ardhi likiwemo Pori hilo ambapo walitoa maelekezo ya kupitia upya kwa mipaka na hatimaye maelekezo hayo kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Aidha,amesema zoezi la utatuzi wa mgogoro husika lilikuwa shirikishi kwa kufanya vikao mbalimbali vilivyohusisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nyasa pamoja na wananchi ambapo wananchi wa vijiji husika waliteuliwa katika zoezi zima la uwekaji vigingi na kufanikiwa kujenga jumla ya vigingi 140 kuzunguka hifadhi hiyo.

Akizungumzia hatua hiyo, mkazi wa Kijiji cha Liparamba Bw. Eligius Simon Mbawala ambaye pia alikuwa fundi wa kujenga vigingi aliyeteuliwa na wananchi wenzake kushirikiana na wahifadhi katika zoezi zima la kuweka vigingi katika hifadhi ya Liparamba ameeleza namna zoezi hilo lilivyokuwa shirikishi.

"Tumemaliza mgogoro huu mimi nikiwa fundi nimezunguka Pori zima la Liparamba ukianzia mpaka wa mitomoni hadi ndondo yote nimepita kuzunguka na kujenga hizo "beacon" (vigingi).

"Mpaka tulipo hapa leo tunafurahi, na tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mama Samia kwa kumaliza huu mgogoro vizuri na watu sasa wanaendelea kufurahi na kunufaika na maeneo haya kwa kazi zao za kiuchumi na maendeleo ya kijamii kwa ujumla,"amesema.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja amesema,pamoja na maelekezo mengine, Serikali ilitoa maagizo kwa Mamlaka zote zinazohusiana na Hifadhi nchini kushirikisha wananchi katika maeneo yote ili kuwe na mapitio ya pamoja ya mipaka ili kila mwananchi ajue mpaka uko wapi, na pia kuweka vigingi kama alama inayoonesha pande zote mbili.
Amesema, TAWA imetekeleza kikamilifu maagizo hayo na mapendekezo yote ya BLM na kuwasihi wananchi kuheshimu mipaka ya hifadhi hiyo huku akisisitiza mashirikiano ya pande zote mbili katika kulinda rasilimali zilizopo ndani ya hifadhi hiyo

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news