UASIN GISHU-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Rigathi Gachagua amesema, ana uhusiano mzuri wa kikazi na Rais Dkt.William Ruto.
Pia, amesema kuwa Rais Dkt.Ruto amempa majukumu ya kutosha kuondoa uvumi kwamba uhusiano wao unayumba.
Mheshimiwa Righati Gachagua ambaye siku chache zilizopita aliwakashifu baadhi ya wanasiasa wa Rift Valley kwa kuingilia siasa za Mlima Kenya alitaja uhusiano wake na Rais Dkt.Ruto kama uhusiano wa hali ya juu unaolenga kuimarisha amani na umoja kote nchini.“Mimi na Rais Ruto tuko katika uhusiano mzuri, kwa kweli Rais amenipa majukumu mengi kama naibu wake na lengo letu kwa sasa ni kuwaunganisha Wakenya wote hasa wale ambao waliingiliwa na hofu wakati wa uchaguzi mkuu uliopita,” amesema Gachagua.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika Shule ya Msingi ya Matharu katika Kaunti ya Uasin Gishu wakati wa kuchangisha fedha za kusaidia makanisa 15 kutoka eneo hilo,Makamu wa Rais huyo alitoa wito kwa Wakenya wote kuunga mkono Serikali ya Kenya Kwanza.
Mheshimiwa Gachagua ambaye amekuwa akipiga kambi katika Kaunti ya Uasin Gishu kwa siku tatu zilizopita alisema amejitolea kumuunga mkono, Rais Dkt.Ruto katika azma yake ya kuwaunganisha Wakenya wote.
“Nimekuwa katika kaunti hii kwa siku tatu zilizopita kwa sababu ya maendeleo na kuwashukuru kwa kuunga mkono Serikali yetu.
"Jukumu letu kuu ni kuwaunganisha Wakenya wote ili kuchochea maendeleo,” alisema Makamu wa Rais, Gachagua akihutubia katika soko la Burnt Forest baada ya harambee. (NA)