Mkopo changamkia

NA LWAGA MWAMBANDE

SERIKALI kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, imetenga shilingi bilioni 18.5 kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara ndogondogo nchini kwa riba nafuu kupitia Benki ya NMB.

Hayo yamebainika Mei 6,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya miaka miwili kati ya wizara hiyo na Benki ya NMB.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akishuhudia tukio hilo, alisema, kutokana na umuhimu wa sekta hiyo, Serikali imechukua hatua kuhakikisha inaimarishwa ikiwemo kuwapa fursa ya kupata mikopo ya kuwawezesha kuinuka kiuchumi.

“Tukumbuke nia ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha ustawi wa wafanyabiashara ndogondogo ilianza tangu 2022 alipounda wizara na kuweka kundi hili kwenye wizara hii.

"Aidha, alitoa fedha ya kujenga ofisi za Machinga kila mkoa na kuelekeza wapewe maeneo. Hivi sasa mikoa tisa imekamilisha ujenzi wa ofisi na mingine ofisi ziko hatua mbalimbali za ujenzi,” alisema Waziri Dkt. Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima amewataka wote watakaokopeshwa fedha hiyo wajue kuwa watatakiwa kurejesha pamoja na riba kidogo ambayo imewekwa ili kusaidia usimamizi na uendelevu na kufanya mkopo huo kuwa na tija na hatimaye wafanyabiashara wengi watafikiwa na kunufaika.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande licha ya kupongeza juhudi kubwa za Serikali katika kuhakikisha ustawi bora wa wananchi wake, pia anawahimiza wafanyabiashara ndogondogo kuchangamkia fursa. Endelea;

1.Kuna mambo ni mazuri, hata kwa wabishi watu,
Tuseme wazi tukiri, Serikali ina kitu,
Wewe hebu ufikiri, na hii mikopo yetu,
Biashara ndogondogo, mkopo changamkia.

2.Wawafaa wamachinga, na biashara za vitu,
Hapa pale wanapanga, hawabakii pale tu,
Mbele waweza kusonga, kuzalishazalisha tu,
Biashara ndogondogo, mkopo changamkia.

3.Waendeshaji bajaji, hata pikipiki zetu,
Mikopo mkihitaji, ipo Serikali yetu,
Sema yenu mahitaji, mwaipata roho kwatu,
Biashara ndogondogo, mkopo changamkia.

4.Mama nawe baba lishe, kilipo chakula chetu,
Na nyie msijichoshe, hizo papatupapatu,
Mikopo jielimishe, mnaweza kukopa tu,
Biashara ndogondogo, mkopo changamkia.

5.Wizara Maendeleo, Jamii Jinsia zetu,
Wanawake wa kileo, Makundi maalum yetu,
Imetoa matokeo, kutujali hali zetu,
Biashara ndogondogo, mkopo changamkia.

6.Usijione mdogo, muhimu kwa nchi yetu,
Hivyo wachoma mihogo, ndipo tunaponea tu,
Kopa na uwe kigogo, milionea wa kwetu,
Biashara ndogondogo, mkopo changamkia.

7.Hili la kuzingatia, hizo pesa ni za kwetu,
Za kwetu Watanzania, tujenge uchumi wetu,
Kopa na kisha tumia, kuijenga nchi yetu,
Biashara ndogondogo, mkopo changamkia.

8.Pale utakapokopa, pesa hizo fanya kitu,
Zalishazalisha lipa, kisha zifae wenzetu,
Wala usijekusepa, bila kurudisha chetu,
Biashara ndogondogo, mkopo changamkia

9.Na cha kukopa kiwango, ujikadirie mtu,
Huo wala si mpango, kupatapata pesa tu,
Kukopa huo ulingo, ongeza zalisha kitu,
Biashara ndogondogo, mkopo changamkia.

10.Asante kwa Serikali, hii inajali watu,
Kweli imeona mbali, kukumbuka hawa watu,
Kwenye uchumi ni mali, kwa maendeleo yetu,
Biashara ndogondogo, mkopo changamkia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news