NA MARY GWERA
Mahakama Ghana
CHAMA cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) Ukanda wa Afrika kimehitimisha Mkutano wake huku kikitoka na maazimio kadhaa ikiwemo kuwataka Wanachama kutoka Ukanda huo kuhakikisha kuwa Sheria, Kanuni na desturi ndani za nchi zao zinawiana na Haki za Binadamu na dhamana za kikatiba.
Sehemu ya Washiriki wa Mkutano wa 18 wa Chama cha Majaji Duniani 'IAWJ' Ukanda Afrika wakiwemo Wanachama kutoka Tanzania wakifuatilia hotuba ya ufungaji wa Mkutano huo iliyokuwa ikitolewa na Rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani 'IAWJ' Tawi la Ghana, Mhe. Rita Agyeman-Budu (hayupo katika picha).
Akizungumza wakati akifunga Mkutano wa 18 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) Ukanda wa Afrika katika Hoteli ya Labadi jijini Accra nchini Ghana, Rais wa Chama hicho tawi la Ghana, Mhe. Rita Agyeman-Budu aliwasisitiza washiriki wa mkutano huo kutekeleza yote waliyojadiliana na kukubaliana.
Rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani 'IAWJ' Tawi la Ghana, Mhe. Rita Agyeman-Budu akifunga Mkutano wa 18 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) Ukanda wa Afrika uliofanyika katika Hoteli ya Labadi jijini Accra nchini Ghana.
“Nachukua fursa hii kuwapongeza washiriki wote mliohudhuria katika mkutano huu, hivyo nawaomba tuungane sote kwa pamoja kuvunja tamaduni hasi na za kibaguzi ambazo zinasababisha ukiukwaji wa haki za binadamu,” alisema Mhe. Rita.
Mkutano huo ulioanza tarehe 13 Mei, 2024 ulihudhuriwa na Wanachama wa IAWJ kutoka Nchi takribani 14 ambazo ni pamoja na Tanzania, Nigeria, Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Botswana, Senegal, Cote D’voire na nyingine.
Akisoma maazimio ya Mkutano huo, mmoja wa Sekretarieti ya Maandalizi, alieleza miongoni mwa maazimio hayo ni pamoja na ushirikishwaji wa Watawala wa kimila ili kuleta mabadiliko kwa kuwaelimisha juu ya haja ya wao kuepuka kuingilia Mchakato wa Mahakama hasa unapohusisha makosa ya kujamiiana na uhalifu dhidi ya watoto na wanawake.
Jaji Mkuu wa Ghana, Mhe. Gertrude Sackey Torkornoo akitoa neno la shukrani kwa Washiriki wa Mkutano wa 18 wa Chama cha Majaji Duniani 'IAWJ' Ukanda Afrika (hawapo katika picha) uliofanyika jijini Accra nchini Ghana.
Azimio lingine ni Viongozi wa Kimila wanapaswa kufunzwa kuwawezesha wanawake na walio katika Mazingira hatarishi katika jamii zao kwa kuwa wanaheshimiwa na kuchukuliwa kama Viongozi wa kutoa ushauri na maoni.
Maazimio mengine yaliyofikiwa katika Mkutano huo ni kila Nchi Wanachama kuwa na Rejesta ya Wahalifu wa Kujamiiana ambayo inapaswa kuhuishwa mara kwa mara ili kusaidia kufuatilia na kubadilishana taarifa miongoni mwa Nchi Wanachama ili kupambana na makosa ya kingono yanayohusiana nayo.
Majaji na Mahakimu hao wanawake wamekubaliana pia kuelimisha na kutoa mafunzo kwa waliotengwa na walio katika mazingira hatarishi juu ya Mifumo ya Kisheria ya Nchi Wanachama na upatikanaji wa haki.
Jaji Mkuu wa Ghana, Mhe. Gertrude Sackey Torkornoo (aliyesimama mbele) akiwa amevalishwa Khanga maalum aliyopewa zawadi na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Barke Sehel (wa tatu kushoto). Kulia ni sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao pia ni Wanachama wa TAWJA walioambatana na Mhe. Sehel kutoa zawadi hiyo kwa Jaji Mkuu wa Ghana.
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Barke Sehel (wa tatu kushoto) akitoa zawadi ya Khanga kwa Rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani 'IAWJ' Tawi la Ghana, Mhe. Rita Agyeman-Budu (wa pili kulia).
Kadhalika, waliazimia kufuatilia na kuchambua hoja za Mahakama. Huku kila Nchi Mwanachama wa ‘IAWJ’ inapaswa kuwa macho katika kuhakikisha kuwa dhana potofu hazizuii upatikanaji wa haki kwa waathiriwa/wanusurika wa unyanyasaji wa kijinsia.
Maazimio hayo na mengine yote yalijielekeza katika mlengo wa Kaulimbiu ya Mkutano wa mwaka huu iliyosema; Nafasi ya Majaji Wanawake katika kupambana na mila potofu katika ulimwengu wa sasa.’ Kupitia Kaulimbiu hiyo Wanachama wa ‘IAWJ’ walisisitizwa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu vitendo mbalimbali vinavyoakisi mila potofu.
Sehemu ya Wanachama wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani 'IAWJ' wakisaini makubaliano 'Communique' ya Mkutano wa 18 wa Chama hicho Ukanda wa Afrika.
Baadhi ya Wanachama wa TAWJA wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ratiba ya kufunga Mkutano wa 18 wa Chama cha Majaji Duniani 'IAWJ' Ukanda Afrika uliofanyika katika Hoteli ya Labadi Accra nchini Ghana.(Picha na Mary Gwera, Mahakama ya Tanzania).
Mada zilizotolewa katika Mkutano huo ni pamoja na ya Ukatili wa mtandao; je Watoto wetu wapo salama, umaskini na upatikanaji wa haki, kuondosha dhana hasi dhidi ya wanawake-wajibu wa Majaji, ushiriki wa wanawake katika Utawala wa Taasisi za Manispaa na kitaifa na nyingine.
Mkutano ujao wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) unatarajia kufanyika Aprili, 2025 nchini Afrika Kusini.