MOROGORO-Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Morogoro (MOROPC) katika mkutano wake mkuu kimezindua mkakati wa kiubunifu wa kuendeleza taasisi hiyo ya kitaaluma mkoani hapa iliyosajiliwa zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Nickson Mkilanya,Mwenyekiti wa chama hicho alibainisha mapema kwenye mkutano mkuu wa mwaka uliofanyika katika ukumbi wa Bwalo la Umwema JKT,ambapo mkakati wa kiubunifu ni mbinu shirikishi za kuweka historia ya kipekee ya kuendeleza chama hicho ili kiweze kujitegemea.
Mkilanya amewashawishi wajumbe wa mkutano mkuu kutambua umuhimu kutimiza wajibu wao katika kuchangia maendeleo ya chama ikiwemo kuibua miradi mbalimbali itakayohusisha jamii na kuchochea stori za mabadiliko.
Kadhalika, alihimiza suala la ujenzi wa jengo la chama ili kuleta mabadiliko ya kifikra kutokana na mawazo ya kutegemea wahisani pekee jambo ambalo linaongeza udumavu wa maendeleo ya kitaasisi.
Kwa upande wa wajumbe wa mkutano mkuu waliungana na hoja ya kujitegemea katika mchakato wa ujenzi wa jengo la ofisi ambalo ahadi mbalimbali zilitolewa kwa kila mwanachama wameonesha kuchangia mifuko kati ya miwili hadi 10 ya saruji sanjari na fedha tasilimu.
Morogoro Press Club ina jumla ya wanachama zaidi ya 120 ambapo wamejiwekea mkakati ifikapo Juni 2025 jengo la ofisi litakuwa limekamilika.
Katika mkutano huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambapo mwakilishi wake, Sajeti Benjamini Bandula alitumia fursa hiyo kuwapongeza waandishi wa habari kwa kutimiza wajibu wao wa kuelimisha na kupasha habari umma juu ya kukabiliana na majanga yanapotokea.
Sanjeti Bandula aliwahakikishia waandishi wa habari kuwa Jeshi la zimamoto litaendelea kushirikiana na waandishi wa habari katika shughuli mbalimbali za kijamii na kuwaelimisha wananchi jinsi ya kuchukua hatua za awali katika kukabiliana na majanga ikiwemo ya asili.
Alisema Mkoa wa Morogoro,kama ilivyo katika maeneo mengine nchini,katika maeneo ya Kihonda,Kilosa,Kilombero na Mlimba yalikumbwa na mafuriko kutokana na kuwepo kwa mvua zilizokuwa juu ya wastani hivyo elimu kwa umma inahitajika kutolewa kupitia vyombo vya habari kwa kuzingatia mamlaka ya hali ya hewa.