Mwinjilisti Temba amtabiria Edgar Chagwa Lungu kurejea madarakani Zambia

DAR-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba amemtabiria Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu kurejea madarakani kwa nafasi ya urais tena.

Ni kupitia Uchaguzi Mkuu wa Zambia ambao unatarajiwa kufanyika mwaka 2026.

Mwanasiasa huyo na Rais wa Awamu ya Sita ambaye alizaliwa Novemba 11, 1956 alihudumu nafasi ya urais Zambia kuanzia Januari 26, 2015 hadi Agosti 24,2021.

Kupitia utabiri wake wa Machi 15, 2024 Mwinjilisti Temba amesema,Mungu amemuonesha Lungu anakwenda kupokea kijiti kutoka kwa Rais Hakainde Hichilema ambaye alimkabidhi madaraka Agosti 24,2021.

Pengine, utabiri huu unakuja kipindi ambacho Zambia ambayo ilikuwa ina matumaini makubwa kutoka kwa mfanyabiashara, mkulima na mwanasiasa, Hichilema kuhusu kuinua uchumi na kuboresha ustawi wa maisha yao, mambo yanatajwa yamekwenda mrama.

Mheshimiwa Hichilema ambaye alizaliwa Juni 4, 1962 ni Rais wa Awamu ya Saba ya Jamhuri ya Zambia ambaye atahudumu hadi mwaka 2026, kabla ya Wazambia kufanya maamuzi kupitia sanduku la kura.

Utabiri

Tabiri nyingi za Mwinjilisti Temba zimekuwa na matokeo ya papo kwa papo, hii ni kutokana na karama aliyopewa na Mungu ambayo inamfanya kuwa Mtumishi wa Mungu wa tofauti zaidi.

Mwinjilisti Temba ambaye ametembelea mataifa mbalimbali na kujizolea umaarufu kwa kutoa nabii ambazo zimekuwa zikitimia kama zilivyotabiriwa, katika unabii wake huo amesema, Bwana amemuonyesha kuwa aliyekuwa Rais mstaafu Edgar Chagwa Lungu ambaye alishindwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021 yeye ndiye atakayeshinda kinyang'anyiro hicho katika uchaguzi ujao dhidi ya Rais wa sasa Hakainde Hichilema.

Akiendelea kuzungumzia juu ya uchaguzi huo utakaofanyika nchini Zambia mwaka 2026 ambapo Rais wa sasa Hakainde Hichilema atakwenda kugombea kwa kipindi cha pili na cha mwisho kutokana na Katiba yao, Mwinjilisti Temba ameeleza kuwa, wakati wa Mungu umefika wa kumrudisha tena aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Edgar Chagwa Lungu.

Mwinjilisti huyo wa Kimataifa amebeinisha kuwa Edgar Chagwa Lungu alitokana na matunda yaliyotokana na aliyekuwa Rais wa Zambia, Hayati Michael Sata ambaye anadai kwamba Mungu alikuwa amemfunulia tangu mwaka 2006 kuwa atakuwa Rais wa nchi hiyo na 2011 Michael Sata alishinda kiti cha Urais wa Zambia.
Mwinjilisti wa Kimataifa,Alphonce Temba akimwongoza sala ya toba aliyekuwa Rais wa Zambia mwaka 2011, Hayati Michael Sata katika Ofisi ya Ikulu ya Lusaka nchini Zambia.

Ameendelea kusema kwamba sababu hiyo kuna kauhusiano japo wakati Edgar Chagwa Lungu akiwa Rais, hakuwa karibu naye na wala hakuwahi kumtembelea, lakini lipo agano la Kimungu ambalo alilifanya katika Ikulu ya Lusaka nchini Zambia pamoja na Hayati Rais Michael Sata.

Akifafanua zaidi Mwinjilisti Temba amesema kuwa, Lungu ana uwezo wa kumchagua mtu mwingine kuendelea kama atapenda kwenye chama chake kama yeye akipenda kupumzika, lakini ni kwamba bado nyota inamuwakia Lungu kushinda uchaguzi huo.

Kwamba pamoja na Rais huyo wa sasa wa Zambia Hichilema kuwa ndiye tajiri namba moja wa Zambia kwa kuwa na kiasi cha dola milioni 389, utajiri wake huo hautaweza kumsaidia kushinda urais huo.

Hata hivyo amesema, alivyowasili Zambia na kupokelewa na Mwenyekiti wa Chama cha Rais wa sasa Hichilema cha United Party for National Development (UPDP), Stephen Katuka, alimwambia amfikishie ujumbe Rais kutokuhamia Ikulu kabla hajamuombea na kukutana naye.

Alimwambia wazi kuwa Rais huyo alipaswa amuone haraka amuombee na kumjulisha Agano la Mungu katika Ikulu ya Lusaka na endapo asingemwita na kuingia ndani na kuishi Ikulu mauti ingempata.
Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba akiwa na Mwenyekiti wa Chama Tawala nchini Zambia cha United Party for National Development (UPDP), Stephen Katuka alipowasili nchini humo. (Picha na Maktaba).

Hivyo, akamuonya amwambie Rais amuite kama anataka kuwa salama kitendo ambacho Rais aligoma kumuita na cha ajabu aligoma kuhamia katika Ikulu ya Zambia, mpaka sasa Rais wa Zambia Hichilema anaishi katika makazi yake nyumbani kwake Lusaka nchini Zambia.

Alipoulizwa kuwa Nabii zake zimekuwa kubwa na za kimatifa na kwa nini siku hizi hatoi Nabii za nchi ya Tanzania ambapo mambo yamekuwa ni mengi hususani katika mitandao ya kijamii na mambo mengine mengi, huku Uchaguzi Mkuu kwa Tanzania ukitarajia kufanyika mwakani 2025, lakini ameruka hadi Uchaguzi wa 2026 tena wa nchi nyingine,

Mwjilisti wa Kimataifa Temba amesema kwamba, ni kweli kuna uchaguzi mwaka huu wa Serikali za Mitaa na kuna uchaguzi 2025, Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais, lakini amejikita kwa sasa kutoa unabii juu ya Mataifa mengine nje ya Tanzania.

Kwamba ametoa maelekezo kuwa aulizwe nchi yoyote ile itakayofanya Uchaguzi iwe ndani ama nje ya Afrika ataendelea kutoa unabii juu ya nani atakayekwenda kushinda kiti hicho cha urais na kusisitiza kuwa kwa sasa hatatoa unabii wowote juu ya Tanzania.

Akinukuu maandiko katika Bibilia kitabu cha Marko 6:2 alisema, "Na ilipokuwa Sabato, alianza kufundisha katika Sinagogi, wengi waliposikia wakashangaa, wakisema huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake?.

Akiendelea Kunukuu Marko 6:3,anasema "Huyu si yule, Seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni?, Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake, huku Marko 6, Mlango wa nne akinukuu kuwa "Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake".

Huku Marko 6:5 ukisema "Wala hakuweza kufanya mwujiza wowote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya,".

Hivyo baada ya kusoma maandiko hayo Mwinjilisti Temba amesema, ni kweli Mungu amekuwa akimuonyesha mambo makubwa juu ya Tanzania na mambo mengine, na hakuna Nabii yeyote ambaye amekwisha yatamka na hadi sasa anayo.

"Lakini kwa sababu ndani ya Taifa la Tanzania, wapo watu Serikalini na Ndani ya Chama Tawala ambao wamenidaharau kwa kuniona kwamba ni mtu asiye maana, nimedhalilishwa, nimetukanwa, nimedhalaurika," amesema Mwijilisti Temba.

Hivyo amebainisha kuwa Kitabu cha Marko kinaonesha wazi kwamba Yesu alipopitishwa kwenye maneno hayo katika andiko hilo hilo, anasema maandiko yanasema hakufanya miujiza katika mji wake kwa sababu ya dharau.

Kutokana na hali hiyo Mwinjilisti Temba amedai kuwa kuanzia sasa ataendelea kujikita kutoa Unabii Mkubwa juu ya Mataifa mbalimbali nje ya Tanzania, kwa sababu alidhalilika kama vile Yesu alivyodhalilika kwenye mji wake ambapo Yesu baada ya kudhalilishwa alichofanya aliwaacha na hukutenda miujiza tena kwenye mji wake.

Amesema kwamba, na yeye hatatoa unabii tena juu ya Taifa la Tanzania ambalo viongozi wakiwepo na baadhi ya watu wengine wamekuwa wakimdhalilisha, kumtukana na kumdharau.

Hata hivyo amesema kuwa yapo mambo ambayo ameyaona juu ya Tanzania ambapo kwa sasa wengi wanakimbilia kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu, na wengine wakikimbilia kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025 ambapo wengi wanaangalia kwenye ushindi wa kiti cha Urais na Ubunge ambapo yeye anasema anaona tofauti na wanavyoangalia watu wengine.

Akinukuu katika Bibilia, Daniel 2:21 anasema, "Yeye hubadili majira na nyakati; huzuru wafalme na kuwamilikisha wafalme; huwapa hekima wenye hekima; huwapa wenye ufahamu maarifa."

Mwinjilisti Temba amebainisha kuwa,Serikali ya Awamu ya Nne ya Tanzania inajua mchango wake, kwani hata aliulizwa mambo na viongozi wakubwa wakiwa nje ya nchi na yeye ndiye alimtambulisha Nabii Mkuu wa SCOAN, T.B Joshua, kwa Serikali ya Awamu ya Nne.

Hata hivyo amesema nchini,Botswana ambapo mwaka 2024 utafanyika Uchaguzi Mkuu Chama Tawala cha Botswana Democratic Party (BDP) Chini ya Rais wa sasa wa Awamu ya tano Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi ataibuka mshindi, lakini huenda akakabiliana na tatizo kubwa la kiuchumi kwa mashinikizo ya kimkataba au kesi za kibiashara juu ya biashara ya Almasi na kukawa na punguzo kubwa la wafanyakazi na kuumiza uchumi wa Botswana.

Kwamba hiyo ni kutokana na maamuzi yaliofanywa na Rais Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi, katika sakata hili litafungua upinzani mkubwa sana na huenda ukawa mwanzo wa vyama vya upinzani kupata nguvu kubwa sana nchini humo.

Hata hivyo Mwinjilisti Temba ameendelea kusema kwamba katika nchi ya Zambia unabii alioutoa ni kwamba Edgar Chagwa Lungu anakwenda kushinda Uchaguzi Mkuu wa 2026, na kwamba anakwenda kuwasiliana naye hivi karibuni ili aweze kumpa nafasi ya kumweleza unabii huo juu ya ushindi atakaokwenda kupata katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Kwamba endapo Lungu atakubaliana na Mwinjilisti Temba, ni kwamba Mtumishi huyo wa Mungu atamfanyia maombi makubwa ambayo yatamsaidia kumpa nguvu na ulinzi wa Malaika kuwa juu yake ambapo vurugu na maonevu havitaonekana tena kwake kwa sababu ipo neema ambayo Mungu alimpa kwa ajili ya kusaidia viongozi ambao ni watiifu juu ya neno la Mungu.

Ameendelea kueleza kuwa,baada ya unabii huo kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao wa Zambia ataendelea kutoa Unabii juu ya Mataifa mengine na kuwatolea unabii viongozi wa Mataifa hayo na pale atakapoalikwa na kukubalika kwenda atakwenda kwa gharama zake,kwani huduma ya Mungu anayofanya sio ya kulipia bali anaitoa bure.

Kwa mawasilano na Mwinjilisti wa Kimataifa Alphonce Temba: Emaili, phonce2003@yahoo.com

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news