Ni tabasamu kwa wataalam wastaafu Wizara ya Ujenzi

DODOMA-Wizara ya Ujenzi kupitia taasisi zake Bodi ya Usajili Wahandisi (ERB) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) inaandaa utaratibu wa kutumia wataalam wa ndani waliostaafu katika ujenzi na matengenezo ya barabara.
Waziri wa Ujenzi,Mheshimiwa Innocent Bashungwa ameyasema hayo leo Mei 29,2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25.

Amesema,hatua hiyo ni katika kujenga uwezo wa ndani wa taasisi na wastaafu wabobezi katika usimamizi wa miradi badala ya kutegemea wataalam kutoka nje.

“Tumeanza utaratibu wa kutumia wataalam wa ndani waliostaafu yaani retired but not tired katika ujenzi na matengenezo ya barabara.”

Amesema, Kitengo cha Ndani cha Ushauri wa Kihandisi cha TANROADS (TECU) kinaendelea kuwatumia wahandisi wabobezi waliostaafu katika usanifu na usimamizi wa miradi.

“Hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza utegemezi wa wahandisi washauri kutoka nje. Jambo hili la kutumia wastaafu pia linatoa fursa kwa wataalam wanaochipukia na ngazi ya kati kujifunza kutoka kwa wastaafu wabobezi ambao wako nyumbani wakati ujuzi wao bado unahitajika katika ujenzi wa taifa letu.”

Amesema,TANROADS inatumia TECU katika usanifu na usimamizi wa miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja.

“Hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za usimamizi wa miradi pamoja na muda unaotumiwa katika ununuzi wa wahandisi washauri.”

Amesema, TECU imeshiriki kwa mafanikio katika utekelezaji wa miradi kadhaa ya kimkakati, ikiwemo Mradi wa Uzalishaji wa Umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Njia 8 ya Kimara-Kibaha (km19.2), Mradi wa Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Geita, na ujenzi wa kiwanda cha sukari cha Mbigiri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news