DODOMA-Mganga Mkuu wa Serikali,Prof. Tumaini Nagu ametoa maagizo lwa wataalamu wa Afya kushirikiana ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Prof. Nagu amesema hayo leo 17 Mei, 2024 wilayani ya Kondoa mkoani wa Dodoma wakati akipokea taarifa ya Huduma za kibingwa na Ubingwa Bobezi zinazoendelea katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa.
"Wananchi asilimia 70 mpaka 80 wanapata huduma za Afya kwenye ngazi ya msingi, tumeona changamoto kama gharama, umbali hivyo Serikali tukaona ni vema tuwasogezee karibu huduma za kibingwa na bobezi kwenye maeneo yenu,"amesema Prof. Nagu.
Prof. Nagu amesema, Serikali inatambua Kazi kubwa wanayoifanya Madaktari hao ndio maana imeendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma kwenye ngazi zote ili huduma zinazotolewa ziwe bora kwa manufaa ya wananchi na serikali kwa ujumla.
Prof. Nagu amewahimiza wataalamu wa afya kutumia ujuzi huu waliopata kwenye kambi na wajinoe kila wakati ili iweze kuwasaidia katika utaoji wa huduma.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amesema katika kutekeleza azma ya Serikali kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi, Wilaya ya Kondoa ilipokea madaktari Bingwa na Bingwa bobezi 5 kwenye maeneo tofauti ya Huduma za ambao wanatoa huduma za mkoba za kibingwa na ubingwa bobezi.
Amesema, muitikio wa wananchi umekua ni mzuri mpaka Tarehe 16, Mei 2024 hospitali ya Wilaya ya Kondoa imehudumia wananchi zaidi ya 1,190 ambapo amesema Madaktari Bingwa hawa pamoja na Kutoa huduma za kibingwa wanatoa mafunzo elekezi kazini (Mentorship) kwa wataalamu wetu katika Hospitali za halmashauri.