Rais Dkt.Samia atoa neno leo Siku ya Wafanyakazi Duniani

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amewashukuru wafanyakazi wote nchini kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa ustawi bora wa Taifa.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa shukurani hizo leo Mei 1,2024 ikiwa ni Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo Kitaifa imeadhimisha jijini Arusha.

Katika maadhimisho hayo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amewakilishwa na Makamu wa Rais. Mheshimiwa Dkt.Philip Isdor Mpango ikibebwa na kaulimbiu isemayo Nyongeza ya Mshahara ni Msingi wa Mfano Bora na Kinga Dhidi ya Hali Ngumu ya Maisha.

Aidha, Kidunia imebebwa na kaulimbiu isemayo Ensuring Safety and Health at Work in a Changing Climate 2024.
"Kheri ya Siku ya Wafanyakazi kwenu nyote. Siku hii ni ya mambo makubwa mawili.

"Jambo la kwanza ni kwa sote kuwashukuru wale ambao kwa kazi zao sisi kama Taifa tunaweza kusonga mbele; kuanzia dada wa kazi hapo nyumbani anayeamka mapema alfajiri kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa, hadi daktari anayehakikisha tunapata tiba pale tunapokuwa na changamoto ya maradhi. Tunawashukuru nyote katika kila kona ya nchi yetu. Ahsanteni kwa kazi.

"Jambo la pili, leo pia ni siku ya kurudia ahadi yetu kwenu. Ahadi ambayo kila wakati tumekuwa tukiitoa na kuitekeleza kadiri tuwezavyo.

"Ahadi kwamba kama Serikali tutaendelea kutekeleza jukumu letu la msingi kuhakikisha mazingira ya kazi yanazidi kuwa bora zaidi kwa kila mmoja si tu mishahara, bali pia haki katika maeneo ya kazi, kupanda madaraja kwa wakati, kupata stahiki sahihi na uboreshaji wa mifumo yetu ya pensheni,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news