NA LWAGA MWAMBANDE
MWEZI Aprili, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan alitoa kibali cha ajira zaidi ya watumishi 20,000 kati yao 13,130 walikuwa wa kada ya ualimu kwa ajili ya kufundisha elimu ngazi za msingi na sekondari.
Vile vile, kati ya hao 7,192 walikuwa ni waajiriwa katika Sekta ya Afya huku vituo vya afya 367 vikijengwa nchini, dhamira ikiwa ni kuendelea kuhudumia jamii kwa ustawi bora wa afya na maisha yao.
Hatua hiyo muhimu imefikiwa ikiwa pia, Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inatarajia kuajiri watumishi wapya 46,000 katika kada ya Elimu,Afya na kada nyingine kabla ya mwezi Juni, mwaka huu baada ya Rais Dkt.Samia kutoa kibali hicho Aprili 16, 2024.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene aliyasema hayo Aprili 17,mwaka huu bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu kwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI,wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Bernadeta Mushashu aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kupeleka walimu katika shule za msingi na sekondari.
“Rais ametoa kibali cha kuajiri watumishi 46,000 na katika idadi hiyo kibali cha ajira ya walimu ni 12,000 na ajira ya Afya ni zaidi ya 10,000 na imani yangu kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI tutahakikisha upungufu wa walimu kwenye maeneo yetu tutakwenda kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa na tunafikiria kuwa na utaratibu mpya wa kuajiri kupitia kwenye mikoa yetu na katika kuzingatia maoni ya wabunge,"alibainisha Mheshimiwa Simbachawene.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande ampepongeza hatua hiyo, huku akibainisha huku juhudi hizo za Mheshimiwa Rais Dkt.Samia zinalenga kustawisha jamii.Endelea;
1.Tunaojua hesabu, jumlisha na kutoa,
Tayari tuna majibu, mashaka kuyaondoa,
Anatimiza wajibuu, changamoto kuondoa,
Rais wetu Samia astawisha jamii.
2.Ikifanya Serikali, Rais hutamwondoa,
Pale juu mhimili, maelekezo atoa,
Ribiti zikiwa kali, kitu huwezi kutoa,
Rais wetu Samia, astawisha jamii.
3.Ni mambo ya Tamisemi, ajira amezitoa,
Kuwasomesha wasomi, ili waweze tutoa,
Miaka yake hakomi, walimu anawatoa,
Rais wetu Samia, astawisha jamii.
4.Tusimseme Samia, miongozo anotoa,
Kwani twasahaulia, wahitimu livyopotoa,
Miaka ilivyoishia, bila nafasi kutoa?
Rais wetu Samia, astawisha jamii.
5.Hasa kwa sisi wahanga, watoto walivyopoa,
Uwalimu kujipanga, ujinga kuuondoa,
Nyumbani wakajipanga, bila ya kodi kutoa,
Rais wetu Samia, astawisha jamii.
6.Alfu kumi na tatu, na zaidi atatoa,
Ajira walimu wetu, elimu kwenda kutoa,
Kule kwa watoto wetu, ujinga kuuondoa,
Rais wetu Samia, astawisha jamii.
7.Walimu kuajiriwa, kiwingu anaondoa,
Kwamba wanathaminiwa, mchango wao kutoa,
Serikali yaelewa, kazi yanayoitoa,
Rais wetu Samia, astawisha jamii.
8.Na watumishi wa afya, elfu saba tatoa,
Magonjwa ya kuogofya, wapambane kuyatoa,
Vingi vituo vya afya, upungufu kuondoa,
Rais wetu Samia, astawisha jamii.
9.Ikifanya Serikali, Rais wetu ni poa,
Kweli anaona mbali, ajira anavyotoa,
Uwekezaji halali, maduhuli utatoa,
Rais wetu Samia, astawisha jamii.
10.Hao watalipa kodi, paye yao kuitoa,
Huduma tapiga hodi, kupata pesa watoa,
Ni kutimiza ahadi, ilani ilizotoa,
Rais wetu Samia, astawisha jamii.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602