DODOMA-Wakala wa Nishati Vijijini (REA); unategemea kusambaza huduma ya umeme kwenye vitongoji 31,532 vilivyobaki nchini ili kuharakisha upatikanaji wa huduma za nishati kwa madhumuni ya kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa vijijini.
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy ametoa takwimu hizo Aprili 30, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akitoa wasilisho kuhusu Mpango wa Kuharakisha Upelekaji wa Umeme katika Vitongoji vya Tanzania Bara mbele ya Waheshimiwa Wabunge katika ukumbi wa mikutano wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
“Ili kufikisha huduma ya umeme kwenye vitongoji 31,532 vilivyobaki, kunahitajika kujengwa njia za umeme wa msongo wa kati zenye urefu wa kilomita 41,593 na kilomita 87,206 za msongo mdogo, kufunga mashine umba (transformers) 31,532 na kuunganisha wateja wa awali 1,552,343 ambapo mradi huu utagharimu jumla ya shilingi bilioni 6,701.75,” alisema Mhandisi Saidy.
Kwa upande mwingine, Mhandisi Saidy amewaeleza wabunge kuwa kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2020,REA imekamilisha jumla ya miradi mikubwa ya Gridi ya Taifa 15 na inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa 7 ya kupeleka umeme vijijini iliyoanzishwa katika kipindi cha mwaka 2021.
“Baada ya kukamilika kwa miradi hiyo 7, jumla ya vitongoji 9,480 na wateja wa awali 534,906 wataunganishwa na huduma za umeme kupitia ujenzi wa kilomita 26,379 za njia za umeme msongo wa kati na kilomita 26,145 za njia ya msongo mdogo, pamoja na usimikaji wa mashineumba (Transformer) 9,161 kwa gharama ya shilingi trilioni 2.3,”amesema Mhandisi Saidy.
Mkurugenzi Mkuu ameongeza kuwa,lengo la kuanzishwa kwa REA wakati huo lilikuwa ni kuwezesha na kuharakisha upatikanaji wa huduma za nishati bora vijijini kwa madhumuni ya kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa vijijini.
Pia,kuchangia ipasavyo katika ukuaji wa uchumi, kuboresha huduma za jamii, kuhifadhi mazingira na kuimarisha usawa wa kijinsia na hali ya upatikanaji wa umeme.