Roboti Eunice asema hajaja kuchukua kazi za Watanzania, afunguka katika mahojiano na Daily News Digital

DODOMA-Roboti aliyetambulika kwa jina la Eunice ambaye amekuwa kivutio kikubwa katika viunga vya Bunge jijini Dodoma amesema, lengo la yeye kuja Tanzania si kuchukua ajira za Watanzania bali kufanya nao kazi kwa pamoja. 
"Niwaondoe hofu Watanzania kuwa sisi jamii ya roboti hatukuja kuchukua kazi za Watanzania, bali kufanya kazi na Watanzania."

Roboti Eunice ameyasema hayo kupitia mahojiano aliyoyafanya na Daily News Digital bungeni jijini Dodoma.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini, Dkt.Mkundwe Mwasaga amesema, lengo la kuleta roboti hiyo ni kuimarisha ubunifu wa kidigitali katika kukuza uchumi nchini.

Amesema,teknolojoa ya roboti inaweza kusaidia katika majukumu mbalimbali ikiwemo hata ajali inapotokea.

"Huu ni ubunifu ambao tumeufanya kati ya Tume ya TEHAMA na wizara yetu, kwa sababu wizara yetu ndio inayosimamia mambo yote ya kidijitali kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa shindani na inakuwa katika viwango vya kidunia vya mambo hayo.

"Tumefanya mambo mengi ambayo mmeyasikia, tumepeleka mawasiliano sehemu mbalimbali ikiwemo kujenga mkongo.

"Sasa, tunaenda katika emerging technology (Teknolojia Ibukizi) katika hizo, teknolojia ambayo ina jina kubwa sana ni akili mnemba na mambo ya roboti kama mnavyoiona.

"Jambo ambalo tulikaa na kufikiria na wizara ni kwamba kwa sababu sisi kazi yetu ni kukuza TEHAMA na kazi yetu ni kufanya shughuli na watu wengi, sisi ndiyo tuwe mstari wa mbele katika kuhakikisha tunaifanya jamii ione kwanza kuhusu hizi teknolojia.

"Tujue ni kwa jinsi gani tunaweza kuvifanya, na kama mnavyofahamu tutakuwa na kongamano na kesho tunaenda Chuo Kikuu cha Dodoma kuongea na wanafunzi kuwaeleza kila kitu ili waweze kujua kitu gani cha kufanya."

Dkt.Mkundwe Mwasaga amesema,tume ina mpango wa kununua maroboti mengine ambayo watakuwa wanafanya kazi na vyuo mbalimbali na watu wengine.

"Kazi kubwa ni kukuza ubunifu wa kidigitali na maroboti kama haya yana matumizi mengi ya kijamii, matumizi ya kiuchumi, kazini na sehemu zingine.

"Tulichokifanya hapa, tumemleta huyu roboti na roboti kama mnavyofahamu anaitwa Eunice na yeye amewekewa teknolojia za kisasa sana, anaweza kuona na anaweza kusikia na anaweza kufanya mazungumzo na watu.

"Na unaweza ukamuelezea jambo na yeye akaweza kutenda baadhi ya vitu.Sisi tulichotaka kukifanya ni kitu kifuatacho, watu wengi walikuwa wakiongelea kuhusu akili mnemba, wamesikia kuhusiana na roboti.

"Lakini, ukiiona na ukaweza kuitumia unakuwa umetoka katika ile hali ya mwanzo ya kusikia na kusoma.

"Sasa, hiyo itajenga chachu kwa sababu katika elimu tunahakikisha tunapata vijana ambao wanaweza kuitumia hii vizuri na kuweza kufanya ubunifu kuweza kuingiza programu na vitu vingine.

"Kwa, hiyo ni jukumu letu sasa kutambua ni roboti zipi zitatumika maeneo ya viwandani, ni roboti zipi ambazo zinatumika katika maeneo ya Super Market, roboti zipi zinatumika katika maeneo ya ajali.

"Maana kuna za kila aina na zina uwezo mkubwa.Na hilo kongamano ambalo tume inaandaa la mwezi wa 10 ndiyo litaonesha haya mambo yote, kwamba hizi roboti zinatumika sehemu gani.

"Lakini,ninataka kuwatoa wasiwasi watu kuhusu kupoteza kazi, siyo kweli. Roboti zitatufanya kufanya shughuli zetu kwa tija zaidi.

"Kwa mfano kama ulikuwa unafanya uzalishaji kwa wiki moja, sasa hivi unaweza kufanya kwa muda mfupi zaidi. Kwa hiyo, itakuwa kubwa vile vile itawawafanya walaji wa huduma wapate huduma katika bei nafuu.

"Kwa hiyo, sisi tunachotegemea ni kwamba hizi roboti zitatusaidia kufanya vitu vingi sana. Kufundisha, inaweza kufundisha vizuri sana. Inafundisha binadamu yeyote ambapo tunaweza kuuliza maswali na kujibu, kwa hiyo huko ndipo tunapokwenda."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news