DODOMA-Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama nchini (ICTC), Dkt.Nkundwe Moses Mwasaga amesema, Serikali imedhamiria kufanya uwekezaji mkubwa katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kustawisha uchumi wa kidigitali nchini.
Dkt.Mkundwe Mwasaga ameyasema hayo hivi karibuni baada ya tume hiyo kufanya ziara Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) jijini Dodoma.
Ziara ambayo ilikuwa mahususi kuwaelezea wanafunzi kuchangamkia fursa ya kushiriki Shindano la Kwanza la Vijana la Afrika kwenye masuala ya Akili Mnemba na Roboti (The African Youth in Artificial Intelligence and Robots Competition).
Shindano hilo litafanyika kwa mara ya kwanza Tanzania kuanzia Oktoba 13 hadi 17, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
"Kuhusiana na mambo ya robotiki, sisi kama Serikali tumenuia katika hilo jambo na haturudi nyuma, Tanzania si muda mrefu zitakuwepo roboti nyingi kwa ajili ya mambo ya ubunifu au mambo ya kufundisha.
"Na tume imepewa jukumu hilo na sisi tume tumelibeba na tutafanya kazi na taasisi mbalimbali na vyuo hasa.
"Kwa sababu tume siyo chuo, kama nilivyosema mwanzo katika jukumu moja tulilopewa sisi na Serikali ni kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa na watekelezaji hasa wa sera ni vyuo, sekta binafsi na mashirika mbalimbali.
"Sisi kama waratibu vitu vile ambavyo vinaweza vikawa vigumu kwa vyuo kuvinunua, sisi ndiyo tunaweza tukanunua tukaziweka katika hizo innovation hubs tunazozijenga mbalimbali ili ziwe na matumizi kwa watu wote, matumizi kwa wanafunzi kwa jamii na vitu kama hivyo,"amesisitiza Dkt.Mkundwe Mwasaga.
Vile vile, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama nchini, Dkt.Nkundwe Moses Mwasaga ziara yao chuo hapo ina umuhimu mkubwa kutoka na ukubwa ikiwemo upekee wa chuo katika kushiriki mashindano mbalimbali kwa ufanisi.
"Kwanza UDOM ni chuo kikubwa kwa namba ya wanafunzi, kwa eneo kilipo na kipo na kipo katika mji mkuu wa Tanzania, kwa hiyo ni jambo muhimu kwetu sisi kuja hapa.
Lakini, pia kwenye mashindano mengi sana, tumejaribu kuangalia siyo mwaka huu, kwa miaka kadhaa, UDOM imekuwa inatoa wanafunzi ambao ni mfano wa kuigwa ukilinganisha na wanafunzi wengine Tanzania na duniani kote.
Kwa hiyo, tulichokuja kukifanya hapa ni kuja kuongea na wanafunzi na kuwaelezea kwanza mashindano, kuwaelezea sisi kama Serikali tunaangalia kitu gani na tunataka vitu gani vitokee kwenye kuujenga uchumi wa kidigitali.
Ukiangalia takwimu za Tanzania, vijana wenye umri kati ya miaka 15 mpaka 34 ni asilimia karibu 33 ya idadi ya watu wa Tanzania. Kwa hiyo, tuna vijana wengi.
Kwa hiyo tumekuja kwenye vyuo kuhakikisha kwamba, tunawapata vijana wengi wanaofanya ubunifu na tunaamini ubunifu utakuwa na tija kwa Tanzania, kikanda na kwa Afrika kwa muda mrefu.
Kwa sababu tukipata vijana kama ulivyowaona leo, wakaanza kufanya ubunifu na wakaamini ubunifu unaweza ukawapa kazi, utakuwa unaifanya Tanzania iwe shindani zaidi katika masoko ya Dunia.
Uchumi wa kidigitali wa Dunia hauna mipaka sasa hivi, na watu ambao tunawategemea ni vijana waweze kutengeneza masuluhisho mbalimbali yaweze kufika zote duniani.
Sasa, haya mashindano yanafanyika Tanzania kwa mara ya kwanza Afrika, kwa hiyo sisi hapa ndiyo tumekuwa pioneers au chipukizi ambao tumeanzisha hili shindano la Afrika na hili shindano litakuwa kila mwaka.
Ni shindano ambalo linapata ufadhili wa NEPAD (AU-New Partnership for Africa’s Development) ya Afrika, AU the Moment Agency kwa hiyo tunataka sisi tunoeshe ushindani mkubwa ikiwezekana tupate zawadi zote ikiwezekana.
Lakini, tunataka kujenga chachu ya kufanya ubunifu kwa vijana wote wa Afrika na tunaamini kabisa vijana kwa vijana wataanza kutengeneza mahusiano mbalimbali ili tuweze kupata bunifu za Kiafrika si tu za Kitanzania, lakini watu wa mataifa mbalimbali wanashirikiana hasa vijana.
Tutazunguka kwenda vyuo vingine kuhakikisha kwamba wanafunzi wa vyuo vingine wanashiriki katika mashindano haya."
Dhamira, Dkt.Mkundwe Mwasaga amesema, ni ili kuweza kufikia lengo la kufanya vema zaidi katika mashindano hayo na Teknolojia Ibukizi kwa ujumla.
"Mwanzo nilikuwa ninasema katika suala la bunifu sisi tunaangalia utatu ambao kuna Serikali, kuna vyuo ambapo ndipo vipaji vinatokea na majibu ya utafiti halafu pia kuna industries ambao huko ndiko zinapozalishwa kazi na zinazosaidia kutengeneza kazi kwa vijana na kuongeza pato kwa Taifa linalotokana na TEHAMA.Kwa hiyo, sisi huo ndio mtazamo wetu,"amesisitiza Dkt.Mkundwe Mwasaga.
Hata hivyo, ili kujenga rasilimali watu endelevu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na taasisi zilizo chini yake imekuwa ikiandaa programu mbalimbali ikiwemo makongamano ya wataalamu wa TEHAMA ili kujadili masuala ya kuendeleza ujuzi wao katika eneo la teknolojia zinazoibukia Akili Mnemba, robotiki na kadhalika.
Aidha,Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU) na Taasisi ya Ele Vate AI, imeanza maandalizi ya Kongamano la Vijana wa Afrika kuonesha bunifu zao na kushindana kwenye maeneo ya masuala ya Akili Mnemba.
Ni shindano linalohusisha vijana ambalo lilifunguliwa toka Februari 29, 2024 kupitia tovuti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Tume ya Tehama pamoja na tovuti ya www.ele-vate.co.za/competition ambapo shindano hili litafungwa tarehe Julai 8, 2024 na washindi watatangazwa Agosti 31, 2024.
Maeneo ambayo yanashindanishwa ni;
i. AI and Innovation in Mining
ii. Futuurist FinTech Solution
iii. Robotics Design
iv. AI and Robotics Healthcare
v. Education Enhancemnennt
vi. Ethical AI
vii. AI and Robotics Agricultural Solutions
viii. Community Impact and Good Governance
ix. Innovations in Constructions and Artecture Industry
x. Open Category
UDOM
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Razack Lukina anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi amesema,
"Kwanza niishukuru wizara na Tume ya TEHAMA kwa kutupa fursa hii kama UDOM ya kuweza kushuhudia na kumuona moja kwa moja huyu roboti.
"Kwetu, sisi ni fursa na ukizingatia kwamba chuo chetu hasa katika masuala ya TEHAMA tumeyapa kipaumbele sana na wanafunzi wetu wanapambana, wanafanya vizuri sana wanapoingia katika mashindano.
"Kwa hii inazidi kujenga hamasa kwa sababu somo la roboti wanafundishwa, kwa hiyo kwao ni fursa pia kwamba inawajengea hamasa kwamba kumbe kuna kitu ambacho tunaweza tukafanya ambacho kinatatua changamoto katika jumuiya nyingi na katika nchi kwa ujumla katika masuala ya TEHAMA,"amesisitiza Prof.Lukina.