Salamu za Jumapili:Ili atupiganie, na sisi tumwelekee

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA katika Biblia Takatifu kitabu cha Kutoka 14:13 na 14:14, neno la Mungu linasema, “Musa akawaambia watu, msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo.
"Kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya."

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande kupitia salamu zake za Jumapili leo Mei 26,2024 anabainisha kuwa,ili Mungu atupiganie basi na sisi yafaa tumwelekee. Endelea;

1.Ni sifa ya Mungu wetu, sisi kutupigania,
Anajali mambo yetu, kama tunamwandamia,
Hata vije vita vyetu, yeye hutusaidia,
Ili atupiganie, na sisi tumwelekee.

2.Macho yake Bwana wetu, yanakimbia-kimbia,
Katika dunia yetu, apate kuangalia,
Yanayotupata watu, na hata kutuzidia,
Ili atupiganie, na sisi tumwelekee.

3.Anajionyesha kwetu, karibu anatujia,
Huyu mwenye nguvu wetu, kifua kutukingia,
Kikija chochote kwetu, yeye akifanyizia,
Ili atupiganie, na sisi tumwelekee.

4.Upende na wewe mtu, Mungu akikwangalia,
Ishi bila utukutu, kufanya akachukia,
Hata upatwe na kutu, uweze kuangamia,
Ili atupiganie, na sisi tumwelekee.

5.Kwa uelekevu wetu, Mungu tukimwangalia,
Pia ucha Mungu wetu, jinsi twamtumikia,
Hatuachi Mungu wetu, jinsi atufwatilia,
Ili atupiganie, na sisi tumwelekee.

6.Anaona mambo yetu, naye anafurahia,
Akagua njia zetu, naye zinamvutia,
Aja kwetu awe wetu, kwetu aweze tulia,
Ili atupiganie, na sisi tumwelekee.

7.Akiwa upande wetu, na Roho kutuvuvia,
Hata utendaji wetu, kwake waweza tulia,
Huyo Roho ndani mwetu, tazidi tusaidia,
Ili atupiganie, na sisi tumwelekee.

8.Akiwapo ndani mwetu, hakuna cha kuzidia,
Kwa yote yajayo kwetu, yeye atatushindia,
Twende na amani yetu, hadi tutapoishia,
Ili atupiganie, na sisi tumwelekee.

9.Twashukuru Mungu wetu, jisi watusaidia,
Yaliyo ya shida kwetu, majibu watupatia,
Mengine kwa macho yetu, na hata ya siri pia,
Ili atupiganie, na sisi tumwelekee.

10.Utukuzwe Mungu wetu, kwako ndiko twatulia,
Wewe ni Muumba wetu, ngome egemeo pia,
Katika maisha yetu, kwako peke twasalia,
Ili atupiganie, na sisi tumwelekee.
(2 Mambo ya Nyakati 16:9a)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news