Sekta ya Uchukuzi ni ya tatu kwa kutunisha akiba ya fedha za kigeni nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Uchukuzi, Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa amesema, Sekta ya Uchukuzi hapa nchini ni ya tatu kwa kuchangia fedha za kigeni kupitia mauzo ya huduma.
Ameyasema hayo leo Mei 6,2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

"Sekta hii ni ya tatu kwa kuchangia fedha za kigeni kupitia mauzo ya huduma kwa maana ya Trade in Services.

"Katika kipindi cha miaka mitatu, mchango wa sekta hii katika fedha za kigeni umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka dola za Marekani bilioni 1.6 mwaka 2022 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 2.4 mwaka 2024."

Mheshimiwa Waziri Prof.Mbarawa amesema hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 50 katika kipindi hicho.

Pia, amesema Sekta ya Uchukuzi imeendelea kutoa mchango mkubwa wa ukuaji wa Uchumi kwa Taifa kwa kuwa ni sekta wezeshi katika kuchagiza ukuaji wa sekta nyingine za uzalishaji zikiwemo sekta za kilimo, madini, utalii, viwanda na biashara.

"Mathalani, katika mwaka 2022 Sekta ya Uchukuzi ilikua kwa asilimia 3.80 na kuchangia katika Pato la Taifa kwa asilimia 6.70."

Ombi

Waziri Prof.Mbarawa katika mwaka wa fedha 2024/25, ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 2.73 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema, kati ya fedha hizo, shilingi 114,744,476,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 2.6 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news