TANGA-Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema, Serikali inaendelea kuwekeza miundombinu mbalimbali katika Sekta ya Elimu ikiwemo katika vyuo vya elimu ya juu ili Vijana wa Kitanzania waweze kupata Elimu bora itakayowawezesha kushiriki katika maendeleo ya Taifa.
Prof. Nombo ameeleza hayo Mei 27, 2024 Jijini Tanga wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya Maadhimisho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal.
Amebainisha kuwa, kupitia maonesho hayo vijana watapata fursa nyingi za kujifunza na kuona Teknolojia mbalimbali za kisasa, na kubadilishana maarifa juu ya masuala mbalimbali ya Elimu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian amesema, ni heshima kubwa kwa mkoa huo kuwa mwenyeji wa Maadhimisho hayo muhimu na ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya Elimu katika mkoa wa Tanga.
Mhe. Balozi Dkt Burian amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele sekta ya elimu na kwamba uwekezaji wa miundombinu unaongeza chachu ya maendeleo ya elimu katika mkoa huo.