Serikali kuendelea kutoa ajira kwa watumishi Sekta ya Afya

DODOMA-Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali inaendelea kutoa ajira kwa watumishi Sekta ya Afya ambapo katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali imetoa kibali cha kuajiri jumla ya watumishi 13,187 katika Sekta ya Afya.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo bungeni Mei 13, 2024 akiwa anawasilisha hotuba yake ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 akielezea utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika utoaji wa huduma za Kinga nchini.

"Hadi kufikia mwezi Machi 2024, Sekta ya Afya ilikuwa na jumla ya watumishi wa afya 126,925 ambao ni sawa na asilimia 57.9 ya watumishi wote 219,061 wanaohitajika katika Sekta ya Afya kulingana na IKAMA,"amesema Waziri Ummy.

Amesema, kati ya watumishi waliopo, watumishi 101,733 sawa na asilimia 80.2 wapo katika ngazi ya afya ya msingi na watumishi 25,192 sawa na asilimia 19.8 wanafanya kazi katika ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa, Kanda, Maalum na Taifa.

Aidha, Waziri Ummy amesema kutokana na kuongezeka kwa vituo vya utoaji huduma za afya, kuongezeka kwa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi, upanuzi wa huduma za afya katika ngazi za vituo vya afya kwa kuweka huduma za dharura za upasuaji kwa akina mama wajawazito wanaojifungua (CEmONC).

Sambamba huduma za Idara za Dharura (EMD) na wagonjwa mahututi (ICU), mahitaji halisi ya watumishi wa afya kwa sasa ni watumishi 348,923 na kufanya upungufu kufikia asilimia 64.

"Katika kukabiliana na changamoto ya sasa ya uhaba wa watumishi, Wizara imewasiliana na Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kupata vibali vya ajira kwa watumishi wa Afya,"amesema Waziri Ummy.

Amesema, hatua nyingine ni pamoja na kutekeleza mwongozo wa ajira za mikataba ya muda mfupi kwa kutumia mapato ya ndani, kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika Sekta ya Afya kwa kuwashawishi kutumia sehemu ya rasilimali fedha zinazotumika katika kutekeleza programu hizo.

"Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, jumla ya wataalam 4,838 waliajiriwa kwa utaratibu wa ajira za mikataba ya muda mfupi kwa kutumia mapato ya ndani ambapo kati yao, watumishi 4,183 wameajiriwa kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa, kanda, maalum na Hospitali ya Taifa Muhimbili na watumishi 655 wameajiriwa ngazi ya afya ya msingi,"amesema Waziri Ummy.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news