MARA-Katika kuhakikisha inakabiliana na changamoto ya uvamizi kwenye migodi mikubwa, Serikali imepanga kutenga maeneo ya uchimbaji na kuwapatia vijana ili wawe na sehemu ya kujipatia kipato.



“Serikali haifurahii hata kidogo uvamizi na migogoro mbalimbali inayojitokeza baina ya migodi na wananchi wanaozunguka maeneo ya migodi hiyo."
Pia, Waziri Mavunde alibainisha kuwa tayari Wizara imefanya mazungumzo na Kampuni ya Barrick ili katika leseni zao za utafiti walizonazo katika maeneo ya Nyamongo, waweze kutenga eneo kwa ajili ya kuwapatia wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti wa awali wa kusaidia wachimbaji hao.
Vilevile, Waziri Mavunde aliahidi kulielekeza Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO) liweze kupeleka mitambo Nyamongo katika maeneo ya wachimbaji wadogo yatakayotengwa kwa ajili ya kusaidia kuchoronga ili kuongeza tija kwenye uchimbaji wao.
Awali, akitoa ufafanuzi kuhusu uvamizi migodini, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Mhandisi Hamad Masauni alitoa wito kwa Jeshi la Polisi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuwataka Askari Polisi kuwa rafiki na jamii kwa ajili ya ulinzi wao na mali zao.

Akitoa salamu za wananchi wake, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara alipongeza jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kutatua kero na changamoto za eneo la Nyamongo, na kuwaomba wananchi kuendelea kuiamini Serikali yao kwa kuwa inaendelea kuwapelekea ya kweli.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Mtambi aliwashukuru Mawaziri kwa kufika uwandani kutatua changamoto za wananchi na kuahidi kuendelea kusimamia maelekezo yote waliyotoa ili kuboresha maisha ya wananchi kwenye maeneo yanayozunguka migodi.