Serikali yafafanua kuhusu msamaha wa kodi kwa vifaa tiba vya mazoezi

DODOMA-Serikali imesema kuwa, msamaha kwenye vifaa tiba vya mazoezi yaani physiotherapy hutolewa kwa hospitali zilizosajiliwa na kuidhinishwa na Waziri wa Afya, ambapo hupatiwa msamaha wa kodi kwa lengo la kuboresha afya kupitia mazoezi, ambayo ni njia bora ya kuzuia magonjwa na kuboresha ustawi wa jumla wa jamii.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Sylvia Fransis Sigula, aliyetaka kujua kuhusu Serikali kupunguza kodi kwenye Vifaa vya Mazoezi kwa kuwa mazoezi ni tiba.

Mhe. Chande alisema kuwa, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2014, kama ilivyofanyiwa marekebisho mbalimbali, imeainisha msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika kipengele cha 6(1) na Jedwali la misamaha lililopo kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 ambapo bidhaa au huduma zilizopewa msamaha wa Kodi ya VAT ni pamoja na vifaa vinavyotumiwa kwa ajili ya tiba.

‘‘Kuhusu kuondoa kodi kwenye vifaa vyote vya mazoezi ushauri umechukuliwa na unaenda kufanyiwa kazi kwani Serikali iko kwenye mchakato wa ukusanyaji wa maoni na hatimaye kutungwa sheria baadaye kupitishwa bungeni, kwa sasa tuangalie zaidi vyanzo vya ukusanyaji mapato kuliko kupunguza vyanzo vya mapato,’’alifafanua Mhe. Chande.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news