Serikali yaonesha dhamira njema kwa wafanyakazi nchini, GST yatoa mshindi

ARUSHA/DODOMA-Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi Duniani kote wameungana kwa pamoja kusheherekea Siku ya Wafanyakazi Duniani ambapo leo Mei 01,2024 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewafurahisha watumishi wa Umma kwa kuonesha nia ya Serikali ya kuendelea kuwapandisha madaraja, kuendelea kuongeza mishahara na kuboresha mazingira ya watumishi.
Dkt. Mpango ameyasema hayo jijini Arusha katika Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani zilizofanyika Kitaifa jijini humo ambapo ameonesha nia ya Serikali ya kuboresha maisha ya watumishi wa Umma na watumishi wa Sekta Binafsi ikiwemo kupandisha madaraja na kuboresha mishahara kwa watumishi wa umma na watumishi wa sekta binafsi hususan kwa watumishi wa kada ya chini.

Amesema, changamoto mbalimbali ambazo zimeikumba dunia ikiwemo vita na majanga ya asili zimeendela kuathiri uchumi wa Taifa kutokana na kuvurugika kwa mfumo wa ugavi na kupanda kwa bei za mafuta, mbolea, chuma na chakula.

Makamu wa Rais amesema Pamoja na changamoto hizo tathmini ya Serikali na ya Taasisi za kimataifa ikiwemo IMF, Benki ya Dunia, AfDB, Moody’s, Fitch na zinginezo zimeonesha kuwa uchumi wa Taifa umekuwa stahimilivu kwa kiasi cha kuridhisha hivyo hali hiyo itakapoendelea kudumu wafanyakazi wawe tayari kunufaika.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kuboresha maslahi ya watumishi kwa namna mbalimbali, ikiwemo kwa kulipa nyongeza ya mwaka ya mshahara ambapo Mwaka 2023/24 kiasi cha shilingi bilioni 153.9 kililipwa na kwa mwaka 2024/25, Serikali imetenga shilingi bilioni 150.8 kwa ajili hiyo.

Pia amesema Serikali imeendelea kuwapandisha vyeo watumishi mbalimbali, ambapo Mwaka 2023/24 jumla ya watumishi 81,515 walipandishwa vyeo na mwaka 2024/25 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 252.7 kwa ajili ya kuwapandisha vyeo watumishi 219,924.

Makamu wa Rais amesema serikali inathamini na kupokea hoja ya kuboresha Kanuni ya ukokotoaji wa mafao ambapo suala hilo ambalo ni la sayansi ya Watakwimu-bima litashauriwa kwa kuzingatia uhimilivu na uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema likizo ya uzazi ni haki ya mfanyakazi na iwapo mfanyakazi atajifungua mtoto au watoto njiti, kipindi cha uangalizi maalumu hakitahesabiwa kama likizo ya uzazi.

Amesema, vilevile mfanyakazi husika ataruhusiwa kutoka kazini saa 7:30 kila siku kwa muda wa miezi sita baada ya kumalizika kwa likizo ya uzazi ili kumpa fursa ya kwenda kunyonyesha. Aidha amesema Serikali ipo katika hatua ya kuifanyia marekebisho Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Sura 366 ili likizo ya uzazi ianze pale mtoto atakapomaliza kipindi cha uangalizi maalum kadri madaktari watakavyothibitisha.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa wafanyakazi nchini kuendelea kutekeleza majukumu kwa bidii, maarifa, uadilifu kwa kutanguliza maslahi ya Taifa mbele kwa kuongeza tija katika utendaji kazi. Amevisihi vyama vya wafanyakazi kushirikiana na Serikali na Waajiri kuhakikisha tija inaongezwa kwenye maeneo ya kazi kwa manufaa ya Taifa na wafanyakazi wenyewe.

Aidha, amewaasa wafanyakazi kuwa mstari wa mbele katika kudai risiti kila wanaponunua bidhaa na kuhakikisha risiti wanazopewa zimeandikwa gharama halisi ili kuiwezesha Serikali kupata mapato zaidi na kupelekea wigo mpana zaidi wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Maadhimisho ya Mei Mosi kitaifa yamehuduhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko, Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Deogratius Ndejembi, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Dkt. Moses Kusiluka, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) Tumaini Nyamhokya, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi John Mongela, Viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, Mahakama, Vyama vya Wafanyakazi pamoja na wafanyakazi sekta binafsi na serikali.
Kwa upande wa Makao Makuu ya nchi jijini Dodoma, Sherehe hizo zimefanyika katika kiwanja cha Jamhuri jijini humo ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameshiriki kama mgeni rasmi wa sherehe hizo.

Pamoja na mambo mengine, Senyamule ametoa salamu za Rais katika sherehe hizo ambapo amesema Rais Samia anawapenda watumishi wote wa Taasisi za Umma na Taasisi binafsi na kuwataka kuwa watulivu wakati Serikali ikifanyia kazi maboresho ya watumishi wote wa Umma na Sekta Binafsi.

Katika hatua nyingine, Senyamule amewataka Watumishi wote nchini kuchapa kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili kuleta ufanisi katika kazi zao kwa lengo la kuleta maendeleo chanya ya Taifa.

Aidha, ndugu Muadhi Mayunga ambaye ni afisa utumishi katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ameibuka kuwa mfanyakazi Hodari katika Taasisi hiyo kwa kutimiza majukumu yake kwa weledi na ufanisi kwa mujibu wa mpangilio wa majukumu yake.
Sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Kitaifa imebebwa na Kaulimbiu isemayo Nyongeza ya Mshahara ni Msingi wa Mfano Bora na Kinga Dhidi ya Hali Ngumu ya Maisha ambapo Kidunia imebebwa na Kaulimbiu isemayo Ensuring Safety and Health at Work in a Changing Climate 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news