NA GODFREY NNKO
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekamilisha ununuzi wa seti 28 za mitambo ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe (Automatic Weather Stations).
Kati ya mitambo hiyo, mitatu imefungwa katika vituo vya hali ya hewa vilivyopo katika viwanja vya ndege vya Mtwara, Songea na Arusha.
Aidha, mitambo 25 inaendelea na maandalizi ya kufungwa katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe, Tanga, Dodoma, Singida, Kilimanjaro, Katavi, Shinyanga, Kagera, Geita, Simiyu, Kaskazini Unguja, Mara na Mwanza.
Hayo yamesemwa leo Mei 6, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Prof.Makame Mbarawa wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Vile vile, Mheshimiwa Waziri Mbarawa amesema, Serikali kupitia TMA imekamilisha ufungaji wa rada za hali ya hewa katika mikoa ya Kigoma na Mbeya na kufikisha jumla ya rada tano za hali ya hewa nchini.
Aidha, utengenezaji wa rada nyingine mbili amesema, unaendelea kiwandani nchini Marekani na inatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2024.
"Rada hizo zitafungwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma na hivyo kukamilisha lengo la muda mrefu la kuwa na rada saba za hali ya hewa nchini.
"Sambamba na hilo, Serikali imeingia mkataba wa kuboresha rada za hali ya hewa zilizofungwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza ili kuendana na teknolojia ya kisasa ya rada za hali ya hewa."
Kuhusu kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kujenga uwezo kwa watumishi, amesema Serikali kupitia TMA imeendelea na ujenzi wa jengo la ofisi ya Kanda ya Mashariki na Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya Tsunami ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 39.
Vilevile, watumishi 74 wanaendelea na mafunzo ndani na nje ya nchi katika ngazi mbalimbali za elimu.
"TMA imeendelea kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ambapo jumla ya tafiti nne zilichapishwa katika majarida ya kimataifa ya kisayansi.
"Idadi hii inafanya tafiti zilizochapishwa na majarida ya kimataifa kuwa nane ndani ya kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2023/24."
Amesema, tafiti hizo ni kuhusu tathmini ya matukio ya hali mbaya ya hewa katika Bahari ya Hindi; tathmini ya ongezeko la joto kwa kipindi kati ya mwaka 1982 hadi 2022.
Pia, tathmini ya hali ya mvua katika vituo vya hali ya hewa nchini; na tathmini ya mabadiliko ya mvua na athari zake katika kilimo kwa nchi za Afrika Mashariki. "Lengo kuu la tafiti hizo ni kuboresha utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini."
Ombi
Waziri Prof.Mbarawa katika mwaka wa fedha 2024/25, ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 2.73 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema, kati ya fedha hizo, shilingi 114,744,476,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 2.6 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Tags
Bunge la Bajeti
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
TMA Tanzania