MOROGORO-Kwa muda mrefu wananchi wa Kata za Ruhembe, Kidodi, Uwembe, Vidunda, Mikumi na Kilolo wameteseka kwa kusafiri umbali mrefu au kuzunguka kwenye mapori ya miwa kufikia huduma za kijamii.

Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengewa, Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mhe. Denis Londo amesema wananchi hao walitumia gharama kubwa katika kuzalisha mazao yao.

"Hadi mkulima anakuja kuuza mazao yale hapati faida kwa kuwa ametumia gharama kubwa wakati wa kupanda na kukuza mazao yake kutokana na kukosekana kwa miundombinu rafiki."
Mhe. Londo ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Daraja la Luhembe ambalo kwa kiasi kikubwa litampunguzia mkulima gharama za uzalishaji.

Akitoa maelekezo wakati wa ziara hiyo, Mhe Mchengerwa aliwataka TARURA Mkoa wa Morogoro kuhakikisha ujenzi wa daraja hilo unakamilika kwa wakati na kuwataka kujenga barabara za lami zenye urefu wa mita 100 kwa kila upande kuunganisha daraja hilo.
"Nimeona ujenzi unaendelea vizuri sasa na mmeniambia kuwa mmepanga kujenga barabara za kuunganisha daraja hilo zenye urefu wa mita 15 sasa niwatake muongeze zifikie mita 100 kila upande."
