Serikali yazidisha mara tano bajeti ya TARURA mkoani Dodoma

DODOMA-Bajeti ya matengenezo na ukarabati wa barabara na madaraja kwa Mkoa wa Dodoma imeongezeka kutoka shilingi bilioni 12.7 mwaka 2020/2021 hadi kufikia shilingi bilioni 66. 2 mwaka 2023/24.
Meneja wa TARURA mkoa wa Dodoma Mhandisi Edward Lemelo akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambapo amesema, malengo yao ni kufikia asilimia 85 ya barabara ziwe zinapatikana mwaka mzima ifikapo mwaka 2025/2026.

Hayo yameelezwa Mei 7, 2024 na Meneja wa TARURA mkoa wa Dodoma, Mhandisi Edward Lemelo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya ofisi yake katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Mhandisi Lemelo amesema, ongezeko hilo la bajeti kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2023/2024 ambalo limeongezeka kwa asilimia 412.77 tangu Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani 2021 limesaidia kuimarika kwa ubora wa mtandao wa barabara za lami kutoka kilomita 171.29 hadi kilomita 309.71.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Mpwapwa,Mhandisi Emmanuel Lukumay ameeleza kwamba katika wilaya yake ndani ya miaka mitatu wameweza kujenga barabara za zege kilomita 14 kulingana na jiografia ya mji huo ambao ni milima na hivyo wananchi wanaweza kupita wakati wote.

“Barabara za changarawe zimeongezeka kutoka kilomita 1,258.65 hadi kilomita 1,827.5 madaraja 19, maboksi karavati 45 na mitaro yenye urefu wa mita 73,822.24 imejengwa, taa za barabarani 470 zimesimikwa, barabara mpya zenye urefu wa kilomita 544.60 zimefunguliwa ambazo hazikuwepo kabisa,"amesema.

Amesema kuwa, mtandao wa barabara zenye hali nzuri zimeongezeka kutoka asilimia 10, Februari 2021 hadi kufikia asilimia 34.70 Machi 2024. 

Vilevile katika kipindi hicho cha miaka mitatu ya Serikali yaAwamu  ya Sita, TARURA Mkoa wa Dodoma imeongeza vitendea kazi pamoja na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.Meneja wa TARURA wilaya ya Chamwino Mhandisi Nelson Magamga ameeleza kwamba kwa kutumia malighafi zilizopo wilayani hapo wameweza kujenga daraja la mawe kwa shilingi milioni 72 na kuweza kuokoa fedha nyingi ambapo wangejenga kawaida wangetumia milioni 216.

“Magari nane mapya yamenunuliwa na kusambazwa katika ofisi za Mameneja wa wilaya na mkoa, ununuzi wa mitambo ya ujenzi wa barabara ikiwemo ‘Motor Grader’, ‘Roller’, ‘Bulldozer’ na ‘Excuvator’ na ‘Loadbed’ vimenunuliwa na kukabidhiwa kwa Meneja wa wilaya ya Chamwino ununuzi wa vitendea kazi ambavyo vimerahisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi wa kazi za Wakala,” amesisitiza.

Mhandisi Lemelo ameongeza kuwa, wakala umetekeleza miradi ya kielelezo ikiwemo ujenzi wa barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba Km 12.6, ujenzi wa barabara ya lami Mwanga-Kisasa-Medeli kilomita 10.7, ujenzi wa barabara ya lami Swaswa-Mpamaa-Arusha Road Jct kilomita 8.2, ujenzi wa barabara ya lami ya mzunguko Mlimwa Km 1.55, ujenzi wa barabara katika Soko la Machinga kilomita 0.6 na ujenzi wa barabara ya kuzunguka makazi ya Waziri Mkuu kilomita 2.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news