Siku 100 za Sungura na maboresho ya kiutendaji MCT

DAR-Siku chache baada ya kutimiza siku 100 kazini, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Ernest Sungura amefanya mabadiliko ya watendaji wa taasisi hiyo yakilenga kuimarisha na kuleta tija kwa Baraza hilo pamoja na sekta ya habari nchini.
Sungura amesema kwamba malengo mahususi ya mabadiliko hayo ni kuhakikisha MCT inachangia katika kuleta mabadiliko ya sekta ya habari nchini. 

“Lengo ni kuboresha utendaji kazi wa Baraza lenyewe kwa kuweka mazingira ya wafanyakazi kufanya kazi kwa ubora,” alisema Sungura katika kikao cha kifungua kinywa na wafanyakazi kilichofanyika Tegeta Mei 13, 2024, Dar es Salaam.

Katika maboresho hayo, Baraza limeajiri Meneja wa Fedha na Utawala, Bi. Rehema Kongola kujaza nafasi iliyokuwa wazi. Bi Kongola ana cheti cha juu cha uhasibu (CPA) kutoka Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi Tanzania (NBAA). Ameanza kazi rasmi tarehe 2 Mei, 2024.

Halikadhalika limemteua Bi. Ziada Kilobo kuwa mkuu wa ofisi ya Baraza Zanzibar na mtalaamu maalum wa uendelevu wa taasisi ambaye pamoja na majukumu mengine ataimarisha utendaji wa ofisi ya Baraza la Habari Zanzibar na uendelevu wa taasisi kwa kuongeza vyanzo vipya vya mapato yatakayolijenga Baraza.

Aidha, Bi Kilobo anatarajiwa kuboresha ufuatiliaji, tathmini ya matokeo ya kazi na uandishi wa taarifa za utekelezaji miradi mbalimbali katika Baraza. Awali, Bi Kilobo alikuwa ni meneja Rasilimali Watu na Utawala katika Baraza, nafasi ambayo imejazwa na Bi. Kongola. Bi. Kilobo anatarajiwa kuripoti katika kituo kipya cha kazi Zanzibar tarehe 27 Mei, 2024.

“Ili kuimarisha ufanisi wetu ni muhimu kuangalia namna tutatumia ubunifu na kutafuta fursa kupata rasilimali za kujiendesha tofauti na njia zile tulizoziea, hivyo, Bi. Ziada kupita nafasi hii mpya moja ya jukumu lake ni kuhakikisha MCT inaongeza vyanzo vipya vya mapato,” alisema Sungura.

Katika hatua nyingine, Baraza limempandisha cheo Bi. Elizabeth Okuli kutoka nafasi ya Katibu muhstasi wa Katibu Mtendaji wa Baraza na ofisa utawala msaidizi kuwa Ofisa Rasilimali Watu na Utawala. 

Bi. Okuli ataanza rasmi kutekeleza majukumu yake mapya tarehe 1 Juni, 2024. Bi. SaumuMwalimu ataendelea kuwa Kaimu Meneja wa Programu za MCT.

Ndani ya siku 100 za utendaji kazi wake Sungura amefanikisha mambo kadhaa yaliyoboresha utendaji kazi wa wafanyakazi lakini pia kuchangia katika tasnia kwa ujumla.

Tarehe 30 Aprili, 2024 aliiongoza MCT kuandaa Kongamano la Wadau wa Habari na Uchaguzi Tanzania lililofanyika huko Dodoma, ambalo pamoja na mambo mengine washiriki katika kongamano walijadili wajibu wa vyombo vya habari katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Mgeni rasmi katika kongamano hilo alikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba.

Wengine waliohudhuria ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndugu Mobhare Matinyi, mwakilishi wa Balozi wa Marekani, Uingereza nchini, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kama vile Jumuiya ya Ulaya, UNESCO, SIDA, IMS, IFES, viongozi mbalimbali kutoka vyama vya siasa wakiwemo CCM, CUF na ACT Wazalendo, wahariri na waandishi wa habari, vyama visivyo vya kiserikali na wanasheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news