LINDI-Changamoto ya usafiri na usafirishaji bidhaa inayowakabili wananchi wanaotumia barabara ya Kiranjeranje kwenda Ruangwa huenda ikafikia tamati baada ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi kutangaza kuweka kambi eneo hilo ili kuhakikisha njia inapitika.
Kambi hiyo inalenga kuondoa tabu wanayokutana nayo wananchi kwa sasa katika usafirishaji wa bidhaa wanazozalisha na hata wasizozalisha kutokana na kulazimika kutumia bodaboda, kwani hakuna gari inayoweza kupita.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Emil Zengo alipokuwa akieleza mikakati waliyonayo katika urejeshaji wa mawasiliano yote yaliyokatika ndani ya mkoa.
Zengo amesema, barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa watu wa Ruangwa na maeneo jirani ikiwemo Nanjirinji kwani ni wakulima wazuri wa ufuta, mbaazi na hata uchimbaji wa madini mbalimbali.
Barabara hiyo ni miongoni mwa zilizoathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha nchini za El-Nino zilizofuatiwa na mvua zilizosababishwa na Kimbunga Hidaya.
“Mvua za El- Nino zilibeba daraja katika Mto Ngurukuru na kukata mawasiliano kati ya Namichiga na Kilanjelanje,” amesema Zengo.
Amesema, kambi watakayoiweka itakuwa kubwa huku wakiomba Serikali kuwaongeza nguvu ili waweze kuhakikisha barabara zote zinapitika muda wote.
“Kwa sasa barabara hii ina maeneo ambayo mvua zinaponyesha yanajaa maji kwa wingi na kuna maeneo ambayo yanahitaji kujengwa madaraja, bajeti ya Serikali itakaporuhusu kama TANROADS tuko tayari kwa muda wowote utakaohitajika kujenga miundombinu ya makaravati na madaraja ili barabara hii iweze kutumika muda wote,” amesema Zengo.
Kufanya hivyo kutasaidia kuunganisha wilaya ya Kilwa Masoko na Ruangwa na kuwawezesha wananchi kusafirisha mazao yao na kupata chakula ambacho hawawezi kulima.