Tanzania, Afrika Kusini mabingwa Soka kwa Shule za Afrika (ASFC)

NA GODFREY NNKO 

MICHUANO ya Kombe la Ubingwa wa Soka kwa Shule za Afrika (ASFC) barani Afrika imefikia tamati Mei 24,2024 jijini Zanzibar baada ya siku nne za mitanange mikali.
Kupitia michuano hiyo ambayo ilipigwa katika Dimba la New Amaan Complex, Tanzania imetawazwa mabingwa mbele ya mashabiki wao wa nyumbani baada ya kuifunga Guinea upande wa wavulana mabao 1-0.

Aidha, Afrika Kusini nayo ilitawazwa mabingwa soka la vijana wa Afrika kwa upande wa wasichana kufuatia ushindi wa mabao 1-1 (5-4) dhidi ya Morocco.

Fainali ya michuano hiyo ya siku nne iliyofanyika kati ya Mei 21 na 24,2024 jijini Zanzibar ilihudhuriwa na Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, ambaye mapema siku hiyo alitembelea Ikulu ya Zanzibar kukutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Kabla ya fainali hizo mbili, pambano kali la kuwania medali ya shaba lilifanyika mchana.

Uganda ilionesha umahiri kwa kuwashinda wenyeji Tanzania katika mchujo wa kuwania nafasi ya tatu kwa wasichana.

Katika mashindano ya medali ya shaba ya wavulana, Senegal na Benin zilitoka sare ambayo ilibidi iamuliwe kwa mikwaju ya penalti, huku Senegal wakiibuka washindi.

Hamisi Yussuf wa Tanzania alitangazwa Mchezaji Bora wa ASFC 2024 kwa wavulana na Meryem Oubella wa Morocco upande wa wasichana.

Mlinda mlango Bora Wasichana ni Sphumelele Zibula wa Afrika Kusini na Wavulana ni Mujahid Juma wa Tanzania, Mfungaji Bora.

Vile vile, Wasichana ni Shadia Nabrye wa Uganda aliyefunga mabao matatu na Wavulana ni Asmara Keita wa Guinea ambao kila mmoja alifunga mabao matatu.

Tuzo ya mchezo wa Kiungwana Wasichana imechukuliwa na Gambia na kwa wavulana ni Afrika Kusini.

Michuano ya CAF ya Shule za Afrika ni ya kwanza katika soka duniani na inaendelea kuwa shuhuda wa matumizi ya kimkakati ya CAF ya soka na elimu katika kuendeleza vijana barani Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news