MALINYI-Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza utekelezaji wa agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa la kurekebisha haraka barabara zilizokatika wilayani Malinyi ili kurejesha huduma kwa wananchi.

“Mheshimiwa Waziri Mchengerwa alitembelea barabara na madaraja yaliyokatika kutokana na athari za mvua na kujionea barabara hii ya Lugala-Misegese ikiwa imekatika na kusababisha magari kutopita na akaelekeza mara moja barabara hii irekebishwe na mimi kama Naibu Katibu Mkuu ninayeshughulikia miundombinu nimefika nione hali ipoje na tunarekebishaje haraka,kwani Waziri alitoa pia maelekezo kwamba fedha zitolewe, fedha zipo na mkandarasi apatikane kurekebisha eneo hili."
Aidha, amesema moja ya barabara iliyopata changamoto ni barabara inayoenda kwenye hospitali ya wilaya kutokana na dharura hiyo imebidi wamchukue mkandarasi aliyepo jirani afike na aanze kufanya kazi na tayari mkandarasi huyo ameanza kupeleka vifaa kama alivyoagiza Mhe.Waziri kwa kutoa siku nne mkandarasi apatikane na aanze kazi kuhakikisha panapitika.

Vile vile ameiagiza TARURA kusimamia kazi hiyo usiku na mchana ili ikamilike haraka na mkandarasi aweke wafanyakazi na vifaa vya kutosha.
Naye, Katibu Tawala Wilaya ya Malinyi, Bi. Saida Mhanga amesema barabara ya Malinyi - Igawa wanaitumia kuelekea ofisini na nyenzo kuu inayotumika hivi sasa ili waweze kufika kazini ni pikipiki. Hivyo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea milioni 800 kwa ajili ya kurekebisha mawasiliano wilayani hapo.

Mhandisi Charles Mang’era Meneja TARURA Wilaya ya Malinyi amesema wilaya hiyo ni kati ya wilaya ambazo zimepata madhara makubwa kutokana na mvua za masika zilizoanza Novemba mwaka jana mpaka katikati ya Mei mwaka huu hivyo miongoni mwa madhara ambayo yamejitokeza katika wilaya yao ni miundombinu kukatika.
“Takribani kilomita 53 za barabara zimepata madhara ya kukatika, miongoni mwa ambazo zimeathirika zaidi ni hii ya Malinyi – Igawa na Lugala –Misegese, Serikali imekuwa sikivu wametupatia shilingi milioni 800 fedha za dharura kuhakikisha barabara zote mbili zinafunguka na wananchi wanapata huduma.”
Wakati huo huo Mkurugenzi wa ufundi kutoka kampuni ya Bavaco Mellezier Limited Mhandisi Nkolate Ntije amesema tayari wameshapeleka vifaa muhimu kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa kurejesha mawasiliano ya barabara hizo na kuongeza kwamba wanaishukuru Serikali kwa kuwaamini na kuahidi kukamilisha kwa muda waliopewa.
