DAR-Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limepokea taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuhusu uwepo wa kimbunga “HIDAYA” katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya nchi yetu.
Kimbunga “HIDAYA” kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi yetu ambapo hadi kufika saa tisa usiku wa tarehe 03 Mei 2024 kilikuwa kimeimarika zaidi na kufikia hadhi ya Kimbunga kamili kikiwa umbali wa takriban Kilomita 401 mashariki mwa pwani ya Mtwara.
Tangu wakati huo, kimbunga HIDAYA kimeendelea kuimarika zaidi huku kasi ya upepo ikiongezeka hadi kufikia Kilomita 130 kwa saa.
TASAC inawataarifu wadau wote wa usafiri kwa njia ya maji kuwa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini bado unaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga “HIDAYA” kusalia katika hadhi ya Kimbunga kamili kwa saa 12 zijazo huku kikiimarika, na kendelea kusogea karibu kabisa na pwani ya Tanzania.
Kimbunga hiki kinatarajiwa kuendelea kuwepo hadi tarehe 06 mwezi Mei 2024 na kupungua nguvu baada ya tarehe 6 Mei 2024.
Uwepo wa kimbunga hicho utasababisha ongezeko la mvua na upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa baharini yatakayosambaa katika eneo kubwa la
mwambao wa bahari yetu.
Kwa msingi huo, TASAC inatoa wito kwa wadau wote wanaofanya shughuli za kiuchumi,wakiwemo wavuvi, kuchukua tahadhari na kujiepusha kufanya shughuli hizo baharini hadi hapo kimbunga kitakapopita katika mwambao wa bahari yetu.
Kwa vyombo vinavyofanya shughuli za usafirishaji abiria, tunawaasa kuchukua tahadhari kubwa na kutumia taarifa za hali ya hewa kabla ya kuanza safari.
Aidha, tunawaasa wananchi kwa ujumla kujiepusha na shughuli za starehe katika mwambao wa bahari hadi hapo kimbunga kitakapopita katika mwambao wa bahari yetu.
Imetolewa na
Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu