TASAC:Usalama usafirishaji majini ni kipaumbele chetu

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema kuwa,kipaumbele kikubwa ni kuhakikisha usalama wa vyombo, abiria, mizigo yao pamoja na mazingira yote ya usafirishaji majini.

Hayo yamesemwa Aprili 30, 2024 na Amina Miruko ambaye ni Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) katika kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.
Maonesho hayo ambayo yalianza Aprili 23, 2024 hadi Aprili 30, 2024 yalifanyika viwanja vya General Tyre jijini Arusha na kuratibiwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi nchini (OSHA).

“Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeanzishwa kutokana na mamlaka ambayo ilikuwa ikiitwa hapo awali SUMATRA na SUMATRA ilikuwa ikisimamia na kudhibiti usafiri wa nchi kavu au ardhini pamoja na usafiri kwa njia ya maji au majini.

“Na baada ya hapo, mamlaka hii ambayo ilikuwa inaitwa SUMATRA ikagawanywa yakapatikana mashirika au mamlaka mbili, LATRA ambayo inasimamia na kudhibiti usafiri wa ardhini au nchi kavu na sisi TASAC ambao tupo hapa ambao tunasimamia usafiri kwa njia ya maji."

Amesema, TASAC (Tanzania Shipping Agencies Corporation) imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania Sura ya 415 na kuanza kutekeleza majukumu yake rasmi kuanzia Februari 23, 2018 kufuatia Tangazo la Serikali Na. 53 la Februari 16, 2018.

Majukumu ya shirika ni kusimamia na kudhibiti sekta ya usafiri wa majini, kuwezesha biashara ya usafirishaji majini na kufanya biashara ya uwakala wa meli nchini.

"Kikubwa tunachokifanya ni kuhakikisha usalama wa vyombo, abiria, mizigo yao pamoja na mazingira yote ya usafirishaji."

Kwa upande wa usalama wa abiria, Miruko amesema huwa wanafanya kaguzi mbalimbali kuhakikisha kwamba vyombo husika vinakidhi viwango vya Kimataifa.

“Pia, vyombo hivyo vinakuwa na vifaa vya kujiokolea inapotokewa dharura yoyote abiria anaweza kuokolewa kwa namna yoyote ili kuepuka ajali.

“Lakini, pia tunaposema tunahakikisha usalama wa vyombo ni pamoja na kaguzi mbalimbali ambazo zinakuwa zinafanywa na wataalamu wetu katika vyombo hivi ili kuhakikisha kwamba vyombo vinakuwa salama kwa ajili ya abiria.”

Miruko anafafanua kuwa, jukumu kubwa la TASAC ni kuratibu utafutaji na uokoaji pale inapotokea dharura yoyote.

“TASAC ina kituo cha kuratibu utafutaji na uokoaji pale inapotokea dharura. Kwa hiyo TASAC tunashirikiana na wadau wengine wakubwa kama TPA, Marine Police, Navy Police, Beach Management Unit na wengine wote tunakuwa tunashirikiana kuhakikisha kwamba suala la uokoaji linafanyika kikamilifu ili kuepusha ajali mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza."

Amesema, lengo la wao kushiriki katika maonesho hayo ni kuhakikisha kwamba wanashirikiana na wadau wenzao kutoka serikalini na sekta binafsi kuimarisha usalama mahala pa kazi ili pawe salama kwa wafanyakazi.

“Kutokana na kauli mbiu yetu ambayo inasema ‘athari za mabadiliko ya tabianchi katika usalama wa afya kazini.”
Naye Kisango Bakari Mandari ambaye ni Afisa Ugomboaji na Uhamishaji Shehena kutoka Idara ya Ugomboaji na Uondoshaji Shehena (TASAC) amesema,

“Pamoja na majumu mengine ambayo yameelezewa, Shirika la Uwakala wa Meli lina majukumu ya kibiashara chini ya Idara ya Biashara za Meli.

“Na ugomboaji, majukumu ya kipekee kwenye ugomboaji kuna bidhaa tano.Kwa sasa, tunafanya ugomboaji na uondoshaji wa shehena kwenye kemikali zinazotumika kwenye migodi.

“Madini, kwa maana upande wa madini tunafanya na makinikia, kwa mana tunashughulika na uvumbuaji na uondoshaji wa makinikia.

"Lakini, vile vile tunashughulika na ugomboaji na uondoshaji wa nyara za Serikali, kwa maana ya Government Trophies, lakini vile tunafanya uondoshaji na ugomboaji wa wanyama hai kama walivyoelezewa kwenye Sheria ya Wanyamapori.

“Lakini, pamoja na hilo idara ya tano ambayo tunaihudumia ni vilipuzi pamoja na silaha.Kwa hiyo, chini ya Idara ya Biashara za Meli tunahusika na uingizaji na uondoshaji wa bidhaa hizo ambazo nimezungumzia."
Naye Selina Mukiti ambaye ni Afisa Usafirishaji katika Idara ya Udhibiti Huduma za Usafiri Majini katika Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) amesema, katika idara hiyo wanahakikisha huduma za usafiri majini zinatolewa kwa usahihi na viwango bora.

“Katika kufanya hivyo, tunadhibiti watoa huduma ambao wanatoa huduma katika usafiri wa maji. Watoa huduma hao ni mawakala wa meli, mawakala wa uondoshaji na ugomboaji wa mizigo bandarini.

“Lakini, pia tunawadhibiti wakusanyaji na watawanyaji wa mizigo, tunadhibiti pia watoa huduma ndogondogo ndani ya bandari.

“Tunadhibiti pia uanzishwaji wa bandari, tunadhibiti bandari kavu,tunadhibiti pia wale wanaohakiki mizigo pale bandarini.”

Amesema, katika kuwadhibiti watoa huduma hao wanachokifanya kikubwa ni katika utoaji wa leseni, uhuishaji wa leseni na kufuta leseni.

“Tunaweka viwango vya kutoa huduma na bidhaa, lakini pia tunaweka vigezo na masharti ambayo watoa huduma tunaowadhibiti wanatakiwa kuvifuata wakati wanatoa huduma.

“Pia, tunashughulikia malalamiko na kukiwa na malalamiko yoyote juu ya mtoa huduma na mpokea huduma, ama mtoa huduma na mteja karibu sana TASAC tutashughulikia lalamiko lako ili liweze kuhudumiwa kwa wakati.”

Katika hatua nyingine, amesema pia wanadhibiti tozo na viwango vya malipo katika huduma ambazo zinatolewa kwenye usafiri wa majini nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news