TFRA yawapa wakulima uhakika wa mbolea

DAR-Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imewahakikishia wakulima uwepo wa mbolea kwenye maghala yote nchini ifikapo mwezi Julai, 2024.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku, Louis Kasera wa nne kutoka kushoto, watafiti kutoka PCCB Temeke, Maafisa Ugani wa Temeke, wafanyabiashara wa mbolea na baadhi ya watumishi wa mamlaka wakiwa katika picha baada ya kumaliza kikao cha kujadili matokeo ya utafiti uliofanywa na PCCB Temeke kuhusu Mianya ya rushwa katika mbolea.

Pia, kufuatia mwenendo mzuri wa utekelezaji wa mpango wa ruzuku nchini, kampuni mbalimbali za uingizaji wa mbolea nchini ziko tayari kuingiza kiasi cha tani 70,191.988 kabla ya mwezi Julai,2024 ili kuendelea kuwahudumia wakulima.
Kaimu Mkurugenzi, Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku, Louis Kasera akifuatilia mjadala katika kikao kilichowakutanisha wadau kutoka PCCB- Temeke, Maafisa Ugani na wafanyabiashara wa mbolea wa Wilaya ya Temeke kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Mamlaka tarehe 23 Mei, 2024.

Hayo yamebainishwa Mei 23, 2024 na Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku ya Mbolea, Louis Kasera katika kikao cha kujadili hatua za kuchukua ili kuziba mianya ya rushwa iliyobainishwa na Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa nchini (PCCB) Halmashauri ya Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Akielezea mchanganuo wa uingizaji wa mbolea hizo, Kasera amesema, kampuni ya ETG inaingiza kiasi cha Tani za ujazo 2,999.988 za mbolea ya kukuzia aina ya UREA, tani 13,750 ya mbolea ya CAN na tani 4000 mbolea za kupandia za NPK.

Aidha, ameeleza kuwa, kampuni ya OCP Tanzania itaingiza kiasi cha tani 34,042 za mbolea aina ya DAP wakati YARA wanatarajiwa kuingiza tani za ujazo 4,400 za mbolea ya CAN huku kampuni ya PREMIUM Agrochem ikitarajiwa kuingiza tani 11,000 za mbolea ya UREA.
Kaimu Mkurugenzi, Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku, Louis Kasera (mwenye suti ya kaki) akiongoza mjadala katika kikao kilichowakutanisha wadau kutoka PCCB- Temeke, Maafisa Ugani na wafanyabiashara wa mbolea wa Wilaya ya Temeke kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Mamlaka tarehe 23 Mei, 2024.
Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma TAKUKURU- Temeke, Sabina Isuja akiwasilisha mada ya rushwa mara baada ya majadiliano ya viashiria vya rushwa vilivyowasilishwa TFRA na taasisi hiyo kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wa mpango wa ruzuku ili kufikia adhma ya serikali ya kutoa mbolea za ruzuku kwa wakulima.

Aidha, Louis aliishukuru taasisi ya Kupamana na kuzuia Rushwa kwa utafiti walioufanya uliopelekea Mamlaka kuchukua hatua mapema na kuboresha masuala mbalimbali katika mfumo wa mbolea ya ruzuku ili kuziba mianya ya rushwa.

Amesema pamoja na kutatua changamoto za kimfumo, Mamlaka imeongeza vituo vya mauzo katika maeneo mbalimbali nchini ili kufikisha huduma ya mbolea karibu na wakulima vikiwepo vituo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Temeke.
Kwa upande wake, Mtafiti Francis Luena kutoka TAKUKURU Manispaa ya Temeke ameshukuru kwa ushirikiano walioupata kutoka TFRA uliosaidia kuboresha utendaji wa Mamlaka na kuwafikishia wakulima huduma stahiki.

Amesema maazimio yaliyofikiwa katika kikao hucho yanatekelezeka na ufuatiliaji wake utafanyika ifikapo mwezi Desemba 2025 ili kujiridhisha kuwa uwekezaji uliofanywa na serikali unawafikia walengwa.

Naye, Delphina Wambura, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Temeke ameshukuru kwa kushiriki kikao hicho kwani mada zilizojadiliwa zitatatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili wakulima wa eneo hilo hususani kiasi cha mbolea kinachofungashwa kwani wakulima wao wanalima mashamba madogo madogo na bustani ya mbogamboga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news