PWANI-Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kupitia Kurugenzi ya Mipango, Utafiti na Maendeleo ya Soko imeanza rasmi kikao kazi cha kwanza cha wadau kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali kinachofanya tathmini ya hali ya utumiaji wa huduma za bima kwa mali za Serikali.
Kikao hicho cha Siku Tatu kilichoanza leo Mei 21, 2024 hapa Kibaha Mkoani Pwani kimezinduliwa rasmi na Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, ambaye ameelezea kwa kina kuhusu umuhimu wa kuainisha mali za serikali na kuhakikisha kwamba mali hizo zinakingwa dhidi ya majanga mbalimbali kwa kukatiwa bima.
Wakati wa hotuba yake ya ufunguzi Kamishna amesema, hakuna budi kuwa na wivu mkubwa kwa mali za serikali na kwamba mali za serikali zinapaswa kuwa kwenye hali bora wakati wote hivyo zikikatiwa bima zitaweza kurejea katika ubora wake wa awali kwa kuwa zitafidiwa na kampuni za bima.
Aidha, uwepo wa bima kwa mali za Serikali, kutawezesha ufidiwaji wa hasara za mali au maisha kwa wananchi wanaoathirika na ajali zinazosababishwa na mali za Serikali kama vile magari na vyombo vingine vya moto. Kamishna aliendelea kusisitiza juu ya umuhimu wa tathmini hiyo kwa Mamlaka lakini pia kwa Serikali.
“Miongoni mwa majukumu ya TIRA ni kuishauri serikali kuhusu masuala ya bima hivyo tathmini hii itatusaidia kuishauri vyema serikali yetu kwani tutakua na data sahihi juu ya mali zote na hasara itakayoweza kupatikana kama zisipokingwa na bima."Naye Naibu Kamishna wa Bima Bi. Khadija Said awali, alieleza kuwa kazi hii ya tathmini ya mali za serikali kwa upande wa Zanzibar ilifanywa na kubaini kuwa bado ni taasisi chache zilizoweza kukatia bima mali zake na kusema kuwa TIRA kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea na kufanya tathmini zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango, Utafiti na Uendelezaji Soko, Samwel Mwiru amesema ili kupata matokeo yenye tija, tathmini hii inafanyika kwa kushirikisha wadau kutoka taasisi na wizara nyingine kama vile TAMISEMI, Msajili wa Hazina kwa upande wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, Wizara ya Fedha na Wizara ya Ujenzi.