TIRA yawapa neno wadau wa madini nchini

ARUSHA-Wadau wa Sekta ya Madini nchini wametakiwa kusoma na kuelewa mikataba mbalimbali wanayopewa katika makubaliano kabla ya kuisaini hususani katika taasisi za Bima.Hayo yamesemwa Mei 23, 2024 na Meneja wa Kanda ya Kaskazini TIRA, Bahati Ogolla katika Jukwaa la Tatu la Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini linaloendelea kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano AICC jijini Arusha.

Jukwaa hilo linalofanyika kila mwaka limeandaliwa na Serikali kupitia Tume ya Madini chini ya Wizara ya Madini likiwa na lengo la kukutanisha wadau mbalimbali kutoka Sekta ya Madini kujadili na kufanya tathmini ya ushirikishwaji wa watanzania katika mnyororo wa sekta hiyo.

Akizungumza Ogolla amesema kuwa, wananchi wengi wanakutana na changamoto mbalimbali ya mikataba kwakuwa wanaisaini bila kusoma na kuielewa.

“Someni mikataba vizuri kama huelewi tumia wanasheria au njoo TIRA kwa msaada zaidi, msiingie mikataba bila kujua faida na hasara,”amesema.

Amesema kabla ya kuisaini ni vyema kushirikisha baadhi ya watu ili kushauriana na kuepuka matatizo na maumivu yatakayojitokeza baadaye.

Aidha, TIRA imetoa mapendekezo nane ya kufuatwa ili watanzania waweze kunufaika na huduma za BIMA.
Mapendekezo hayo yaliyotolewa ni pamoja na wananchi kuhakikisha shughuli na mali zinawekewa kinga dhidi ya vihatarishi mbalimbali, kuhakikisha wanalipa ada za bima inavyotakiwa na kuhakikisha wanatambua haki na wajibu wao kwenye mkataba wa bima mfano, ukomo wa muda wa kuwasilisha madai na uwasilishaji wa vielelezo vinavyotakiwa.

Mapendekezo mengine ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanatambua kanuni na taratibu za bima ikiwemo ulipaji wa ada ya bima, uaminifu uliotukuka, uhusiano wa umiliki wa mali na mkatabima kurejeshwa kwenye hali iliyokuwepo kabla ya janga kutokea.

Aidha, ameitaka jamii kushirikiana na mamlaka kufichua vitendo vya udanganyifu kwenye biashara ya bima, mfano, madai yasiyokuwa halali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news