TMA imeendelea kuchagiza shughuli za Uchumi wa Buluu-Prof.Mbarawa

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Uchukuzi, Mheshimiwa Prof.Makame Mbarawa amesema, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kupitia huduma zake imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuchagiza shughuli za Uchumi wa Buluu nchini.

"Serikali kupitia TMA imeendelea kutoa huduma za hali ya hewa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi na maziwa makuu kupitia ofisi zake tisa zilizopo katika bandari za Malindi-Unguja, Mkoani-Pemba, Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Ziwa Victoria katika Bandari ya Mwanza,

"Ziwa Tanganyika katika Bandari za Kigoma na Karema na Ziwa Nyasa katika Bandari ya Itungi na hivyo kuendelea kuchagiza shughuli za Uchumi wa Buluu."
Prof.Mbarawa ameyasema hayo leo Mei 6, 2024 wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 bungeni jijini Dodoma.

Amesema, wadau wa Uchumi wa Buluu ambao wameendelea kupatiwa huduma za hali ya hewa ni pamoja na watumiaji wa vyombo vya usafiri na usafirishaji,watafiti na wachimbaji wa mafuta na gesi.

Wengine ni mamlaka za bandari,wavuvi,wakulima wa mwani na matango bahari, wafugaji samaki na vikundi vya usimamizi wa maeneo ya bahari na fukwe.

Vile vile, amesema kutokana na umahiri katika utoaji wa huduma za hali ya hewa, mwaka 2019 Shirika la Hali ya Hewa Duniani liliichagua Tanzania kupitia TMA kuendesha kituo cha kanda cha kutoa mwongozo wa utabiri wa hali mbaya ya hewa (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo katika ukanda wa Ziwa Victoria.

"Kituo hicho kipo Dar es Salaam na kinahudumia nchi tano ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi. Sambamba na hilo, TMA iliteuliwa kutekeleza jukumu la kufuatilia ubora wa takwimu za hali ya hewa (data) zinazopimwa katika vituo vya hali ya hewa vya nchi sita vya ukanda wa Afrika Mashariki ikujumuisha nchi ya Sudan Kusini."

Amesema, majukumu hayo ambayo TMA imeendelea kuyatekeleza kwa ufanisi na kuzidi kuitangaza nchi yetu kimataifa.

Kwa upande wa sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa, amesema Tanzania kupitia TMA ilifanya vizuri na kuchaguliwa katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa linalosimamia sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa (Intergovernmental Panel on Climate Change-IPCC).

"Hii ni fursa kwa Tanzania kuweza kushiriki katika maamuzi ya Kimataifa kuhusu hali ya hewa pamoja na kupata usaidizi wa vifaa na utaalam."

Ombi

Waziri Prof.Mbarawa katika mwaka wa fedha 2024/25, ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 2.73 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema, kati ya fedha hizo, shilingi 114,744,476,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 2.6 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news