TMA yatoa angalizo Kimbunga IALY katika Bahari ya Hindi

DAR-Kufuatia taarifa iliyotolewa Mei 17,2024 na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu kuwepo kwa kimbunga IALY katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar, mamlaka hiyo imetoa mrejeo kuhusiana na mwendendo wa kimbunga hicho.
Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa, kimbunga hicho kimeendelea kuimarika na bado kimeendelea kusalia katika Bahari ya Hindi kama ilivyotabiriwa awali.

Hadi ilipofika saa 3 asubuhi ya leo kilikuwa umbali wa takriban kilomita 680 mashariki mwa pwani ya nchi yetu.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 19,2024 na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Kutokana na umbali huo kutoka nchini, TMA imeeleza vipindi vya upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita mbili vinaweza kujitokeza katika Bahari ya Hindi hususani kati ya leo tarehe 19 Mei 2024 na Jumanne tarehe 21 Mei 2024.

Vilevile, vipindi vya mvua vinaweza kujitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani hususani kati ya tarehe 21 na tarehe 22 Mei 2024.

USHAURI:

"Watumiaji wa bahari na wananchi wa maeneo ya ukanda wa pwani wanashauriwa kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

"Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news