DAR-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya Mtwara.
Mifumo ya hali ya hewa iliyopo kwa sasa inaonesha kuwa mgandomizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kuimarika na kufikia hadhi ya Kimbunga kamili hadi kufikia kesho tarehe 2 Mei 2024.
Wakati mgandamizo huo mdogo wa hewa ukiendelea kuimarika, unatarajiwa pia kusogea kuelekea baadhi ya maeneo ya pwani ya nchi yetu kuanzia usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa tarehe 3 Mei 2024.
Mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kuendelea kuwepo katika maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi yetu hadi tarehe 6 Mei 2024.
Hata hivyo,mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kupungua nguvu baada ya tarehe 6 Mei 2024.
Uwepo wa mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Dar es Salaam namaeneo ya jirani.
USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa mgandamizo huo mdogo wa hewa na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara kila inapobidi.
Imetolewa na:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
TMA Tanzania