TMA:Kimbunga Hidaya hadi saa tisa usiku leo kilikuwa kilomita 401 Mashariki mwa Pwani ya Mtwara

DAR-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga Hidaya kilichopo katika Bahari ya Hindi Mashariki mwa Pwani ya nchi yetu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 3,2024 saa 3:00 asubuhi Kimbunga Hidaya kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya Pwani ya Tanzania.

"Hadi kufika saa tisa usiku wa tarehe 03 Mei 2024 kilikuwa kimeimarika zaidi na kufikia hadhi ya Kimbunga kamili kikiwa umbali wa takriban Kilomita 401 Mashariki mwa pwani ya Mtwara.

"Katika kipindi hiki kimbunga Hidaya kimeendelea kuimarika zaidi huku kasi ya upepo ikiongezeka hadi kufikia Kilomita 130 kwa saa.

"Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga Hidaya kusalia katika hadhi ya Kimbunga kamili kwa saa 12 zijazo huku kikiimarika, na kendelea kusogea karibu kabisa na pwani ya Tanzania.

"Kimbunga hiki kinatarajiwa kuendelea kuwepo hadi tarehe 06 mwezi Mei 2024 na kupungua nguvu baada ya tarehe 6 Mei 2024.

"Uwepo wa kimbunga Hidaya karibu na pwani ya nchi yetu unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia),

"Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani. Vipindi vya mvua nyepesi na upepo wa wastani tayari vimeanza kujitokeza katika maeneo ya Mtwara. Ongezeko la mvua na upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa baharini vinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani kuelekea tarehe 4 hadi 6 Mei 2024."

USHAURI:

"Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

"Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila baada ya masaa matatu, na mara kwa mara kila inapobidi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news