TMA:Kimbunga Hidaya kimepoteza nguvu wakati kikiingia nchi kavu Kisiwa cha Mafia

DAR-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga Hidaya katika maeneo ya Pwani ya nchi yetu.
Mwenendo wa kimbunga Hidaya unaonesha kuwa mnamo saa 3 asubuhi ya leo, kimbunga hicho kimepoteza nguvu yake kwa kiasi kikubwa wakati kikiingia nchi kavu katika Kisiwa cha Mafia.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 4,2024 saa 10:00 jioni na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Aidha, mawingu ya mvua yaliyokuwa yakiambatana na kimbunga hicho yamesambaa katika maeneo ya Kusini mwa nchi hususani katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na maeneo jirani na kuweza kusababisha vipindi vya mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo.

"Kwa mafano hadi kufika saa 9 mchana, Kituo cha Hali ya Hewa cha Kilwa Masoko (Lindi) kimeripoti mvua ya jumla ya kiasi cha milimita 200.8 kwa kipindi cha masaa 6 yaliyopita.

"Kiwango hiki cha mvua ni kikubwa sana ukizingatia kuwa wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko ni milimita 96.6 tu.
"Hivyo kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya masaa 6 katika kituo hicho ni takribani asilimia 208 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko."

Kwa upande mwingine, katika vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar, Tanga na Dar es Salaam vipindi vya upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa vimeendelea kujitokeza katika nyakati tofauti hadi kufika saa 9 mchana wa leo.

USHAURI:

Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.
"Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na athari zake hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara kila inapobidi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news