TMA:Kimbunga IALY kimepoteza nguvu, hakuna tishio tena

DAR-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imehitimisha mfululizo wa taarifa za kilichokuwa Kimbunga IALY zilizokuwa zikitolewa na mamlaka hiyo tangu Mei 17,2024.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mei 22,2024 saa 4 usiku jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa TMA, mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa katika kipindi cha saa 6 zilizopita, Kimbunga IALY kimepoteza kabisa nguvu yake, kikiwa Kaskazini Mashariki mwa Pwani ya Kenya.

"Hivyo, kwa sasa hakuna tena tishio la kimbunga IALY katika nchi yetu. Aidha, wakati kikipita karibu na Pwani na nchi yetu kati ya jana tarehe 21 na leo tarehe 22 Mei 2024 kimeweza kusababisha vipindi vya mvua, upepo mkali na mawimbi makubwa katika maeneo ya pwani ya nchi yetu kama ilivyotabiriwa awali.

"Hata hivyo ikumbukwe kuwa, japo tunaelekea mwishoni mwa msimu wa Masika, 2024, tunakaribia kuanza kwa msimu wa Kipupwe, na kwa sababu hiyo, vipindi vya upepo wa Kusi baharini vinaweza kuanza kujitokeza na kuambatana na mawimbi makubwa kwa baadhi ya nyakati."

USHAURI

"Wananchi na watumiaji wa bahari wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na maelekezo na miongozo inayotolewa na mamlaka husika."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news