TMA:Kimbunga IALY kipo umbali wa kilomita 500 Mashariki mwa Pwani ya Dar es Salaam

DAR-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa kimbunga IALY katika Bahari ya Hindi.
Kimbunga hicho kwa sasa kipo katika eneo la takribani kilomita 500 mashariki mwa pwani ya Dar es salaam.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 20,2024 saa 10:00 jioni na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Kwa mujibu wa TMA, mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga IALY kinapungua nguvu yake huku kikielekea kaskazini, mbali na pwani ya nchi yetu na kinatarajiwa kuisha nguvu yake kabisa usiku wa kuamkia keshokutwa Jumatano tarehe 22 Mei 2024.

"Hata hivyo, kutokana na umbali kilipo kutoka nchini, vipindi vya upepo mkali vimeanza kujitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani kama ilivyotabiriwa.

Kwa mfano vituo vya hali ya hewa vilivyopo Unguja, Pemba na Mtwara vimeweza kuripoti upepo unaofika kilomita 50 kwa saa katika siku ya leo.

Matarajio ni kwamba, vipindi vya upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita 2 vitaendelea kujitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi yetu na katika Bahari ya Hindi kati ya leo tarehe 20 Mei 2024 na usiku wa kuamkia Jumatano tarehe 22 Mei 2024 kabla kimbunga “IALY” hakijaisha nguvu yake kabisa.

Vilevile, vipindi vya mvua vinaweza kujitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani (mikoa ya Tanga, Pwani (ikijumuisha Mafia), Dar es salaam, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) kati ya Jumanne tarehe 21 na Jumatano tarehe 22 Mei 2024."

USHAURI

"Watumiaji wa bahari na wananchi wa maeneo ya ukanda wa pwani wanashauriwa kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news