DAR-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kufuatia taarifa waliyoitoa Mei 1, 2024 kuhusu uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi Mashariki mwa Pwani ya Mtwara, mgandamizo huo mdogo wa hewa umeendelea kuimarika na kuwa Kimbunga Hidaya chenye nguvu ya kati, kikiwa umbali wa takribani kilomita 506 Mashariki mwa Pwani ya Mtwara.
TMA imesema mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga Hidaya kusogea karibu kabisa na Pwani ya Tanzania kuanzia usiku wa leo Mei 2, 2024 na kuendelea kuwepo hadi Mei 6, 2024, hata hivyo, kimbunga hicho kinatarajiwa kupungua nguvu baada ya Mei 6, 2024.
“Uwepo wa kimbunga Hidaya karibu na Pwani ya Tanzania unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani hususani tarehe 3 Mei 2024 kwa maeneo ya Pwani ya Kusini (Lindi na Mtwara) na kusambaa katika maeneo mengine ya Ukanda wa Pwani kuelekea tarehe 4 hadi 6 Mei 2024.
“Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka TMA, na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza."
Tags
Habari
Kimbunga Hidaya
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)