TPA yahudumia tani milioni 20.72 za shehena ya mizigo bandarini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Uchukuzi, Prof.Makame Mbarawa amesema, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeendelea kusimamia na kutoa huduma zote za kibandari katika bandari zote za Tanzania Bara.

Kutokana na usimamizi huo, hadi kufikia Machi, 2024 TPA ilihudumia tani milioni 20.72 ya shehena ya mizigo ikilinganishwa na tani milioni 14.56 katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 42.31.
Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo Mei 6,2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Aidha, kwa upande wa makasha, amesema TPA ilihudumia makasha 805,167 ikilinganishwa na makasha 688,609 katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 16.92.

"Ongezeko hilo la shehena ya mizigo na makasha limetokana na mikakati mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara."

Pia, amesema Serikali kupitia, TPA imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa bandari nchini pamoja Bandari Kavu.

Aidha, TPA imeendelea na juhudi mbalimbali za kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kufungua ofisi nje ya nchi, kutafuta masoko.

Sambamba na kufanya ununuzi wa vifaa na mitambo kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma katika bandari nchini.

Kuhusu uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Prof.Mbarwa amesema, TPA imeendelea kutekeleza kazi mbalimbali ambapo uchimbaji wa kina umefikia mita 15.5 na upanuzi wa lango la kuingia meli ambalo lina una upana wa mita 200.

Amesema, kwa sasa, bandari ina uwezo wa kupokea meli kubwa zenye urefu wa mita 305.

"Aidha, upembuzi yakinifu wa kuboresha Gati Namba 8 hadi 11 na ujenzi wa Gati Na. 12 hadi 15 bado unaendelea.

"Vilevile, mkataba wa kuendeleza miundombinu ya kupokelea mafuta (Single Receiving Terminal - SRT) unaohusisha ujenzi wa matenki 15 ya mafuta (tank farms) pamoja na miundombinu yake, yenye uwezo wa kuhifadhi kiasi cha mita za ujazo 420,000 umesainiwa Februari 26, 2024 na maandalizi ya kuanza ujenzi yanaendelea."

Amesema,Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imeendelea kushirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa baadhi ya maeneo ya bandari kwa kuingia ubia na kampuni binafsi katika kuendeleza na kuendesha shughuli za bandari kuanzia Gati Na. 4 hadi 7.

"Kwa sasa hatua mbalimbali zikiwemo za makabidhiano na mobilization zinaendelea ili kuruhusu utekelezaji rasmi kuanza."

Pia, amesema Serikali inaendelea na taratibu za kumpata mwekezaji mwingine atakayekuwa na jukumu la kufanya shughuli za uendeshaji kuanzia Gati Namba 8 hadi 11. "Lengo ni kuongeza tija katika utendaji wa bandari."

Ombi

Waziri Prof.Mbarawa katika mwaka wa fedha 2024/25, ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 2.73 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema, kati ya fedha hizo, shilingi 114,744,476,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 2.6 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news