TRC kuanza kutoa huduma Julai mwaka huu Dar hadi Dodoma

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Uchukuzi, Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa amesema, Julai mwaka huu Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) wanatarajia kuanza kutoa huduma kupitia reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
"Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuanza uendeshaji wa treni katika reli ya SGR kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, wizara kupitia TRC inaendelea na majaribio ya miundombinu ya reli kwa ajili ya kuanza utoaji wa huduma hiyo rasmi ifikapo mwezi Julai, 2024.

"Aidha, majaribio haya yanafanyika kwa lengo la kukidhi takwa la usalama kabla ya kuanza uendeshaji."

Prof.Mbarwa ameyasema hayo leo Mei 6,2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Vile vile, amesema Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kusimamia na kuendeleza miundombinu ya reli iliyopo ya Meter Gauge Railway (MGR) yenye urefu wa kilomita 2,706 na kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kutumia reli hiyo.

Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) ya ushoroba wa kati kwa awamu zote mbili ambapo awamu ya kwanza ina jumla ya kilomita 1,219.

Kwa upande wa awamu ya pili ina jumla ya kilometa 1,590 na hivyo kufanya reli mpya ya SGR inayojengwa kuwa na mtandao wenye jumla ya kilomita 2,809.

"Ambazo ni zaidi ya kilomita 103 ikilinganishwa na reli ya MGR ambayo ilijengwa wakati wa Mkoloni."

Pamoja na hatua hiyo, Waziri Mabarawa amesema, Serikali itaendelea na ujenzi wa reli ya SGR kwa maeneo mengine ya Ushoroba wa Kusini na wa Kaskazini kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha.

Amesema,katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali iliahidi kuendelea na ujenzi wa reli ya SGR kwa awamu zote mbili.

"Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, hadi kufikia Machi 2024, ujenzi wa kipande cha kutoka Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 98.93; kipande cha kutoka Morogoro-Makutupora (km 422) umefikia asilimia 96.61.

"Kipande cha kutoka Mwanza- Isaka (km 341) umefikia asilimia 56.21, kipande cha Makutupora -Tabora (368 km) umefikia 14.22%, na Tabora - Isaka (165km) umefikia 5.72%."

Kwa upande wa awamu ya pili, kipande cha kutoka Tabora – Kigoma (Km 506) umefikia asilimia 1.81 na ujenzi wa kipande cha Uvinza – Musongati – Gitega (km 282) umeanza ambapo hatua za ununuzi wa Mshauri Elekezi na Mkandarasi zinaendelea."

TAZARA

Profesa Mbarawa akizungumzia upande wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) amesema,inamilikiwa na Serikali mbili za Tanzania na Zambia kwa hisa za asilimia 50 kwa 50.

Katika kuendeleza huduma za reli kati ya nchi hizo mbili, amesema TAZARA imeendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kutoa huduma za kusafirisha abiria na mizigo.

Pia, kulinda na kuimarisha miundombinu ya reli yenye urefu wa jumla ya kilometa 2,153, na maeneo yote yaliyo ndani ya ukanda wa reli.

Amesema, hadi kufikia Machi 2024, TAZARA ilisafirisha jumla ya tani za mizigo 251,264 ikilinganishwa na tani 235,071 zilizosafirishwa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 6.89.

"Ongezeko hilo limechangiwa na ushirikishaji wa sekta binafsi ya Kampuni Ms Calabash Freight Limited na Ms African Inland Container Depot (AFICD)."

Waziri amesema, utaratibu huo umeiingizia TAZARA mapato ya Shilingi bilioni 8.91 kutokana na kampuni hizo kulipia tozo.

"Treni za abiria zinazofanya safari kati ya Dar es Salaam na New Kapiri Mposhi na ile inayosafiri kati ya stesheni za Kidatu na Makambako zilisafirisha jumla ya abiria 672,006."

Aidha, treni ya jijini Dar es Salaam inayofanya safari zake kati ya Stesheni ya TAZARA hadi Stesheni ya Mwakanga huko Pugu jijini Dar es Salaam amesema, ilisafirisha abiria 1,582,833 ikilinganishwa na abiria 1,447,738 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 9.33.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news