DODOMA-Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka wananchi kuacha tabia ya kuwanyanyapaa wagonjwa wa Afya Akili pamoja na na kuwahi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya mapema.

"Natoa wito kwa Watanzania kuacha kuwanyanyapaa wagonjwa wa akili na kuwahi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya mapema,"amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema Wizara imeendelea kuimarisha huduma za Afya ya Akili kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ambapo inakamilisha mkakati wa utoaji wa huduma za Afya ya Akili na msaada wa kisaikolojia kwa kijamii.
"Magonjwa ya akili yanajumuisha magonjwa yanayotokana na Matumizi ya Dawa za kulevya, Psychoses, kifafa na Neuroses,"amesema Waziri Ummy.
Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi 2024 Waziri Ummy amesema, waliohudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa shida ya magonjwa ya afya ya Akili walikuwa 293,952 sawa na 6.3% ya wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza ikilinganishwa na 246,544 sawa na asilimia 6 kwa kipindi cha mwaka 2022/23.
"Kwa wagonjwa waliolazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya wenye magonjwa ya afya ya Akili walikuwa 19,506 sawa na 7% ya wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza ikilinganishwa na wagonjwa 13,262 sawa na 5% katika kipindi cha mwaka 2022/23,"amesema Waziri Ummy.
Ongezeko hili la wagonjwa wa afya ya akili limetokana na kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu magonjwa haya na kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma.