Tusikubali waiibie Serikali, dai risiti kulingana na kiasi ulichotoa-Mwaipaja

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Fedha imewaomba waandishi wa habari nchini kushiriki kikamilifu kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kulipa kodi ili Serikali iweze kutekeleza miradi ya kimkakati kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa.
"Mwaka huu, Serikali imepanga kukusanya na kutumia shilingi trilioni 49.3 kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo matumizi ya kawaida na maendeleo.

"Kwa hiyo ni namna gani ambavyo tunazipata hizo fedha, tunahitaji mchango wenu mkubwa kama wanahabari kuhamasisha watu kwamba wana wajibu wa kufanya na sisi kama Serikali tuna wajibu wa kufanya ili kuweza kuzipata hizi shilingi trilioni 49.3 kwa mwaka 2024/2025 ambao utaanza tarehe 1 Julai mpaka tarehe 30 Juni;
Hayo yamebainishwa leo Mei 13,2024 mkoani Morogoro na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Wizara ya Fedha, Bw.Benny Mwaipaja wakati akifungua Kongamano la Elimu kwa Wamiliki wa Mitandao ya Kijamii nchini.

Kongamano hilo la siku mbili linaangazia Pensheni na Mirathi na namna bora ya kuripoti taarifa za Bajeti.
"Ninyi kama wanahabari tunaomba mtusaidie mambo machache, lakini kubwa ni kuhamasisha watu kuchangia katika upatikanaji wa hizi fedha.

"Hizi fedha ni za kwao, zinatumika kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ya kimkakati ambayo Serikali inayo.

"Tunajenga sasa hivi miradi ya maji kila mahali, hii miradi ni ya kwao, tunaimarisha masuala ya elimu hizi fedha wanazochangia ndiyo hizo ambazo zinatumika katika kutekeleza hiyo miradi, kuna afya, kuna miundombinu ya umeme.
"Tunataka umeme usikatike, tunafanyaje? Tunahitaji fedha kwa ajili ya kuhudumia hii miradi ya maendeleo.

"Kuna wakati mwingine watu wanasema hii ni bajeti ya kujenga viwanja vya Afcon siyo kweli, mnakuwa hamuitendei haki Serikali.

"Uchambuzi wa kina unatoka kwenu, ninyi wananchi ndiyo wanataka muwadadavulie, bajeti ina maana gani, tunapotaka kusema tunataka kukusanya shilingi trilioni 49.3."

"Hizo zina maana gani kwao, kwa hiyo mtusaidie sana kuhamasisha ulipaji wa kodi, kuhamasisha utoaji wa risiti watu wanapofanya manunuzi muwaambie kwamba mnavyo negotiate risiti maana yake ni kwamba anajipunja mwenye, mfanyabiashara atapata hela na pia ataiibia Serikali hela.
"Lakini, pia unamsababisha aiibie Serikali ndiyo maana tunahamasisha wananchi wadai risiti ambazo zinalingana na kiasi walichotoa. Toa laki moja na ishirini, nunua kitu basi omba risiti yenye thamani ya laki moja na ishirini.

"Kwa sababu, yeye huyo mfanyabiashara ameweka bei yake halafu ameweka asilimia 18 ambazo zinatakiwa ziingie Serikalini.

"Kwa hiyo unapoacha kuchukua risiti maana yake umempa hela zake, lakini pia hela ambazo alikuwa apeleke serikalini. Umemuhonga au umempa hela ambazo siyo zake, kwa hiyo mtusaidie kwa hili.
"Lakini, pia kuwafichua watu wanaokwepa kulipa kodi, ninyi mnafanya investigation journalism, fanyeni investigation mkiona kuna watu wanakwepa basi tupenyezeeni, kwamba mtu fulani anakwepa kulipa kodi ya Serikali...hivi na hivi.

"Kwa sababu ninyi mnakutana na wadau wengi sana mtatusaidia sisi kupata hizi trilioni 49 ambazo tunazihitaji kwa ajili ya maendeleo.

"Nirejee kwa kusema, ninyi ni watu muhimu sana kwetu na ni watu muhimu sana kwa Wizara ya Fedha na ni watu muhimu sana kwa taasisi zetu,"amesisitiza kwa kina Mwaipaja.

Mwenyekiti

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mkutano huo, Mathias Canal ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Wazohuru Media amesema, mkutano huo ni mwendelezo wa mipango ya Wizara ya Fedha kuendelea kukutana na vyombo vya habari vya mitandaoni.
Amesema, mkutano wa awali ulifanyika Oktoba 23 hadi 24, 2023 kwa kuwakutanisha waandishi wa habari wa mitandao ya kijamii ambao wanaandika habari za Wizara ya Fedha.

Canal amesema, mkutano wa mwaka jana ulijenga msingi imara wa wanahabari kuifahamu kwa kina Wizara ya Fedha na majukumu yake, hivyo mwendelezo huu ni hatua muhimu ya kuimarisha msingi huo ili umma uendelee kupata uelewa wa kina kuhusu yanayofanywa na wizara hiyo.
Pia, kupata uelewa umuhimu na faida za kulipa kodi ikiwemo kudai risiti ya kielektroniki pale ambapo anapata au kununua bidhaa popote pale nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news