Tuwafundishe watoto kusaka, kutunza fedha

NA LWAGA MWAMBANDE

MBUNGE wa Kahama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Jumanne Kishimba amesema, kuna umuhimu wa wanafunzi kuanza kufundishwa kutafuta na kutunza fedha kuanzia darasa la kwanza.
Kishimba ameyasema hayo Mei 8,2024 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia Makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

"Mheshimiwa Mwenyekiti kuna somo la kutafuta pesa na kutunza pesa, kwa nini kwenye mitaala halimo?.

"Mheshimiwa Waziri wote hapa mmeeleza... ninataka mwanangu asome akawe daktari, akawe nani ili afanye nini?, si apokee mshahara? Sasa kwa nini tunakataa somo la kutafuta pesa lifundishwe kuanzia darasa la kwanza?.

"Mheshimiwa Waziri litakuwa kosa gani, na madhara yake yatakuwa nini? Yaani madhara ya kutafuta na kutunza pesa yatakuwa nini Mheshimiwa Mwenyekiti?.

"Tunaomba sana wenzetu wa mitaala lazima wakubaliane kwamba suala la pesa liongelewe wazi, kwa sababu ndilo suala la mwisho kote huko kusoma, kufanya nini mwisho wa yote tunakwenda kuangukia kwenye hela. Sasa, kama hatutaki hela tufanyeje? Tutafanya nini bila hela?.

Mshauri wa kisasa Lwaga Mwambande licha ya kumpongeza Mheshimiwa Kishimba kwa mchango huo, pia amesisitiza kuna kila sababu ya watoto kufundishwa kutafuta fedha na kuzitunza.

Dhamira ikiwa ni kuwapa msingi wanafunzi hao ili siku za mbeleni waweza kutawala fedha na siyo fedha iwatawale. Endelea;

1.Jumanne Kishimba, na mheshimiwa wetu,
Kwa hoja huyu ni mwamba, anakonga nyoyo zetu,
Wengi tulio washamba, afungua macho yetu.
Tuwafundishe watoto, kusaka kutunza fedha.

2.Amekuja nayo hii, kwenye lile Bunge letu,
Hekima ya kuitii, kwa maendeleo yetu,
Wanetu wa nchi hii, wawe bora hapa kwetu,
Tuwafundishe watoto, kusaka kutunza fedha.

3.Serikali lenu hilo, na hata nyumbani kwetu,
Elimu si mchapalo, watoke pasipo kitu,
Bali waijue jelo, kuzalisha wawe watu,
Tuwafundishe watoto, kusaka kutunza fedha.

4.Kuwajenga wanafunzi, hiyo hasa kazi yetu,
Biashara wanafunzi, wajue uchumi wetu,
Na viwanda iwe ngazi, kuijenga kesho yetu,
Tuwafundishe watoto, kusaka kutunza fedha.

5.Mawazo ya mweshimiwa, ni mazuri hapa kwetu,
Hasa vile twaelewa, mtaala mpya wetu,
Na mkazo kutolewa, kujenga watoto wetu,
Tuwafundishe watoto, kusaka kutunza fedha.

6.Mafunzo ya darasani, yapo kwa watoto wetu,
Na amali duniani, ziko silabasi yetu,
Hapo wengi twaamini, mema kwa watoto wetu,
Tuwafundishe watoto, kusaka kutunza fedha.

7.Tunawaona wenzetu, hapa na kwao wenzetu,
Watoto ni wadogo tu, lakini wafanya vitu,
Hiyo si bahati tu, bali wanafanya vitu,
Tuwafundishe watoto, kusaka kutunza fedha.

8.Wale wenye biashara, hasa miongoni mwetu,
Kwao itakuwa bora, hizo wawarithishe tu,
Wajifunze barabara, faida kwao na kwetu,
Tuwafundishe watoto, kusaka kutunza fedha.

9.Tunavyomuimba Moo, ni kijana kati yetu,
Kiuchumi ni jogoo, siyo hivihivi katu,
Watu wa wake ukoo, walimwandaa mwenzetu,
Tuwafundishe watoto, kusaka kutunza fedha.

10.Hata wakiondoka, kazi taendelea tu,
Mali haitakatika, anajua kila kitu,
Wetu wakielimika, nasi tutafurahi tu,
Tuwafundishe watoto, kusaka kutunza fedha.

11.Hata sisi wana wetu, wajifunze kazi zetu,
Waache kutumia tu, wajenge uchumi wetu,
Tuijenge leo yetu, hata pia kesho yetu,
Tuwafundishe watoto, kusaka kutunza fedha.

12.Mbunge wetu Kishimba, unakonga nyoyo zetu,
Kujenga hoja ni mwamba, watukugusa mwanakwetu,
Kwake Mungu tunaomba, mambo yako yawe kwatu,
Tuwafundishe watoto, kusaka kutunza fedha.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news