Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura utakuwa na mambo mapya-Kailima

DAR-Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utakuwa na mambo mapya kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwaandikisha wafungwa kwa upande wa Tanzania Bara na wanafunzi wa vyuo vya mafunzo kwa upande wa Zanzibar na kuwaruhusu wapiga kura kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zao kwa njia ya mtandao.
Akizungumza wakati wa mahojiano maalum kwenye kipindi cha Jambo kinachorushwa hewani na kituo cha televisheni cha TBC1 jijini Dar es Salaam leo tarehe 17 Mei, 2024, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima R. K amesema kuwa Tume tayari imeweka utaratibu wa kuwaandikisha wafungwa na wanafunzi hao na mfumo wa kuboresha taarifa mtandaoni upo tayari.

Kailima amefafanua kuwa utaratibu wa kuandikisha wafungwa na wanafunzi utazingatia matwaka ya sheria ambapo waliohukumiwa kifungo cha chini ya miezi sita ndio watakaoandikishwa.

Akizungumzia suala la kuanza mchakato wa uboreshaji wa Daftari mtandaoni, Bw. Kailima amesema Tume imejenga mfumo ujulikanao kama OVRS (Online Voters Registration System) utakaomwezesha mpiga kura anayeboresha taarifa zake kuanzisha mchakato mtandaoni na baadae kwenda kwenye kituo ili amalizie taratibu na kupata kadi yake ya mpiga kura.

Uboreshaji wa taarifa kwa njia ya mtandao una masharti, kwa wale ambao wanataka kurekebisha taarifa zao ni lazima wawe na namba ya NIDA, lakini, mpiga kura anayehamisha taarifa zake hatalazimika kuwa na namba ya NIDA., amesema Bw. Kailima.

Amefafanua kuwa, namba ya NIDA ni muhimu kwa ajili ya kufanya uhakiki wa taarifa za mpiga kura ambazo zinarekebishwa kwenye Daftari.
Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi amefafanua kuwa, wanaokwenda vituoni kujiandikisha kwa mara ya kwanza hawatalazimika kuwa na namba ya NIDA.

Akitoa hotuba ya kutangaza tarehe ya uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari ambao unatarajiwa kufanyika mkoani Kigoma tarehe 01 Julai, 2024, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele alisema kuwa kwa Tanzania Bara kuna vituo vya kuandikisha wapiga kura 130 vilivyopo kwenye magareza na kwa Zanzibar kuna vituo 10 vilivyopo kwenye Vyuo vya Mafunzo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news