Utabiri wa TMA wavuka kiwango cha WMO kwa usahihi

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Uchukuzi, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa amesema, utabiri unaotolewa na Mammlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) umefikia asilimia 86 kiwango ambacho ni juu ya asilimia 70 ya usahihi kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

"Serikali kupitia TMA imeendelea kutoa huduma za utabiri wa kila siku, siku kumi na ule wa muda mrefu pamoja na tahadhari ya matukio ya hali mbaya ya hewa.
"Ni ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao ambapo usahihi wa utabiri umefikia asilimia 86 ambao ni juu ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)."

Mheshimiwa Prof.Mbarawa ameyasema hayo leo Mei 6, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Uchukuzi.

Amesema, miongoni mwa majukumu ya Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ni utoaji wa huduma, kudhibiti na kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini.

Pia, kutoa utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za hali mbaya ya hewa, kupima na kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutafiti kisayansi mabadiliko ya hali ya hewa nchini.

Sambamba na kubadilishana taarifa za hali ya hewa katika mtandao wa mawasiliano wa Dunia kulingana na makubaliano ya Kimataifa na kuiwakilisha Tanzania katika masuala ya hali ya hewa Kikanda na Kimataifa.

Aidha, amesema TMA ilifanyiwa ukaguzi wa kimataifa kuanzia Januari 22 hadi 27,2024 na kuendelea kukidhi vigezo vya kumiliki cheti cha ubora (ISO 9001: 2015).

Ombi

Waziri Prof.Mbarawa katika mwaka wa fedha 2024/25, ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 2.73 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema, kati ya fedha hizo, shilingi 114,744,476,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 2.6 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news