ARUSHA-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), amelihakikishia Shirika la Fedha la Kimataifa (International Monetary Fund-IMF) kwamba, Serikali itaendelea kufanya maboresho ya sera na mipango yake kwa kuhakikisha sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii zikiwemo sekta za elimu na afya zinapewa kipaumbele katika Bajeti ya Serikali.
Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akifunga vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Timu ya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), baada ya kukamilisha tathimini ya awamu ya tatu ya utekelezaji wa program ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii pamoja na maombi mapya ya Serikali ya kupata fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF) kutoka shirika hilo.